NA MWANDISHI WETU DODOMA
SERIKALI imetoa siku saba kwa maeneo yote yanayofanya uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kurekebisha changamoto hiyo na kulielekeza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuyafungia maeneo yatakayokaidi maelekezo hayo.
Mbali na hilo lakini pia imewataka wamiliki wa maeneo ya burudani, starehe na nyumba za ibada kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti ili kuhakikisha jamii zinazozunguuka maeneo hayo haziathiriwi na kelele wanazozisababisha.
Kauli ya Serikali imekuja baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kutoa wito kwa Serikali kutafutia ufumbuzi changamoto ya kelele ambayo imekuwa kero kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kamati hiyo ilitoa ushauri wake Januari 24,2023 jijini Dodoma kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake Kilumbe Ng’enda wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Hata hivyo hatua hiyo imekuja kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya kelele na mitetemo mwaka 2021/2022 ambapo asilimia 65 ya malalamiko yaliyowasilishwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yanahusu kelele na mitetemo, hali inayoonesha adhabu za kutozwa faini kwa wanaokamatwa hazitoshi.
Uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na kelele na mitetemo ni miongoni mwa kero kubwa inayohatarisha afya ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kelele kuwa ni mojawapo ya vitu hatarishi katika maisha ya binadamu na kwa mujibu wa “European Environmental Agency” (EEA, 2018) kelele ni kisababishi cha vifo vya mapema kwa watoto “Pre-mature death”.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 03, 2023 jijini Dodoma,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt.Selemani Jafo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Sura ya 191, Kifungu cha 106 (5 na 6) kinakataza kupiga kelele kuzidi viwango vilivyoruhusiwa na vilevile ni kosa kupiga kelele kinyume na viwango vilivyoruhusiwa.
“Kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015, zimeainisha viwango vya sauti vinavyoruhusiwa kwenye maeneo ya makazi, biashara, viwanda na hospitali ili kulinda afya ya jamii hivyo, nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu kelele na mitetemo kwenye ofisi za serikali za mitaa au ofisi za NEMC,” amesema Dkt Jafo
Aidha, Dkt. Jafo amezitaka Wizara za kisekta, Taasisi za umma, Sekretarieti za mikoa, Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao yaliyoainishwa kwenye mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo wa mwaka 2021.
Itakumbukwa Julai 29, 2019 Serikali ilielekeza kuwa wadau wote wanaohusika kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo inayodhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo na pia hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wale ambao shughuli zao zinasababisha kelele kuzidi viwango vilivyoainishwa.
Hatua za kisheria zilizoainishwa kwenye sheria ni pamoja na kutozwa faini na kufungiwa biashara kwenye maeneo yaliyokithiri kwa kelele na mitetemo.




Discussion about this post