NA MWANDISHI WETU,KATAVI
TANZANIA imepanga kurejesha ekari Milioni 5.2 za Misitu ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni katika juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini.
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera na kimkakati ikiwemo Mkakati wa Kikanda unaojulikana kama (Afri 100) ambao unalenga kurejesha ekari Milioni 100 za misitu na ardhi zilizoharibika.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na Urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Tanzania aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Amesema katika kufikia malengo hayo, Serikali imeanzisha miradi mbalimbali ya mazingira ikiwemo Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mfumo Ikolojia na urejeshwaji wa Uoto Asili na Hifadhi ya Bionuai Tanzania ulioanza mwaka 2021-2025 na kutekelezwa katika Halmashauri za Wilaya saba nchini zilizopo katika Mabonde ya Ruaha Mkuu na Ziwa Rukwa.
Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Mpimbwe, Tanganyika, Sumbawanga, Mbeya, Mbarali, Wanging,ombe na Iringa na kuipongeza Halmashauri ya Mpimbwe kwa juhudi ilizofanya katika kutekeleza mradi huo ikiwemo kutenga ekari 732 kwa ajili ya uanzishaji wa msitu wa hifadhi ya mazingira unaojikita katika uanzishaji wa biashara ya kaboni.
Hata hivyo Dkt.Mkama ameonya kuwa Serikali haitavumilia ubadhilifu wa aina yoyote katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini na itahakikisha kuwa thamani ya fedha inaendana na miradi itakayotekelezwa.
Dkt. Mkama amesema Serikali ya Awamu Sita imekuwa mstari katika kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa watendaji na viongozi waliopo kuhamasisha, kusimamia na kufuatilia miradi hiyo kwani inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Aidha ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ina imani na matarajio makubwa kuona miradi yote ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inachangia ipasavyo juhudi za Serikali katika kuongeza uhakika wa chakula na kuleta maendeleo ya kijamii katika maeneo ya utekelezaji.
“Serikali ya Awamu ya sita inaendelea kutafuta fedha za kutekeleza miradi, natoa rai kwa watendaji na viongozi wa halmashauri zote zinazotekeleza miradi ya mazingira kuhakikisha zinaimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi kuanzia ngazi ya Kata hadi vijiji,” amesema Dkt. Mkama.
Kwa upande wake Mratibu kitaifa wa mradi huo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Damas Mapunda amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021- 2026 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia GEF ukiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 11.2
Ameongeza kuwa mradi huo umelenga kuimarisha usimamizi wa pamoja wa mazingira na urejeshwaji wa ardhi iliyoharibika ili kuleta ustawi wa mifumo-ikolojia.
Aidha amefafanua kuwa kupitia mradi huo, takribani hekta 110,000 za uoto wa asili zinatarajia kurejeshwa nchini ambapo kila halmashauri iliyotekeleza mradi huo imepangiwa eneo lake la utekelezaji kulingana na ukubwa wa jiografia, ambapo hadi sasa Halmashauri ya Mpimbwe imeotesha miche 230,000 ya miti pamoja na kuanzisha mashamba katika shule za msingi.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha IWUKI Wanawake, kilichopo kijiji cha Kikonko Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi Siwema Malima, ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapatia vitendea kazi ikiwemo mizinga ya nyuki ambayo itawasaidia kurinia asali na kuchakata mazao ya nyuki kwa ufanisi na hivyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha jamii kuhusiana na kulinda na kuhifadhi mazingira.




Discussion about this post