NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
ZAIDI ya Wanafunzi 28,981 kati ya 35,732 walioacha masomo wamerejeshwa shule ikiwa ni dhamira ya Serikali ya Mapnduzi Zanzibar kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki yake ya elimu.
Hata hivyo SMZ itahakikisha kuwa Wanafunzi 6,751 waliobaki mtaani wanarudi shule ifikapo 2024 kuendelea na masomo kupitia Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Takwimu hizo zimetolewa Juni 4,2023 Visiwani Zanzibar na Mratibu wa Mradi wa Kuwarudisha Watoto Shule unaotekelezwa Visiwani humo Mzee Shiraz Hassan, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili mbinu bora za kuwarejesha watoto walioacha masomo kurudi shule.
Kikao kazi hicho kilichofanyika katika Shule ya Sekondari Aboud Jumbe Mwinyi iliyopo Fuoni kiliwashirikisha Wenyeviti wa Kamati za Shule na Polisi Jamii wa Wilaya za Magharibi A na Magharibi B.
Amesema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuhakikisha watoto wote nchini wanapatiwa haki yao ya msingi ya elimu kwa ngazi mbalimbali ili kujenga jamii yenye watu wanaojua kusoma na kuandika sambamba na wataalamu wa fani tofauti.
Shirazi,amebainisha kuwa lengo la kikao hicho ni kujadiliana na Wadau hao ambao wapo karibu zaidi na jamii kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi za Wanafunzi walioacha shule ili Waratibu wa Elimu wa ngazi za Wilaya na Mikoa wachukue hatua za watoto hao kuendelea kusoma.
“Jumla ya Wanafunzi 28,981 wamerejeshwa skuli kati ya wanafunzi 35,732 walioacha masomo ikiwa dhamira ya Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ni kuhakikisha Wanafunzi 6,751 waliobaki mtaani ifikapo 2024 watarudi skuli kuendelea na masomo.
“Tunaendelea kuhamasisha jamii yetu na kutoa elimu juu ya umuhimu wa watoto walioacha shule warudishwe na kuendelea na masomo Serikali tayari inafanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha wanasoma bila vikwazo.
“Nitoe wito kwa Walimu Wakuu wanapopelekewa wanafunzi wa aina hiyo waache urasimu wa kuweka vikwazo badala yake wafuate utaratibu uliowekwa na Serikali kwa kesi za aina hiyo ili tufikie dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana na watoto wote wanapata elimu.”,amesema Hassan.
Aidha Hassan amefafanua kuwa watoto wote wenye umri wa miaka saba hadi 14 walioacha shule wamewekewa mazingira rafiki ya kuendelea na masomo na kwamba wale wenye umri wa zaidi ya miaka 15 nao wamewekewa utaratibu maalum kupitia usimamizi wa Elimu Mbadala nchini.
“Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,inaendelea na mkakati wa kuwarudisha shule watoto wote huku wakisaidiwa vifaa vikiwemo sare,madaftari na vitabu na kupewa elimu bure”amesema Hassan
Hata hivyo Hassan ameziomba Kamati za shule pamoja na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi nchini,kutoa taarifa za watoto walioacha masomo na kubaki mitaani ili warudishwe shule kuendelea na masomo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Elimu Mbadala Zanzibar Waziri Rajab Hamza, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua juhudi ya kuwarudisha watoto hao shule ili waendelee na masomo hivyo jamii inatakiwa kuunga mkomo juhudi hizo kwa kuhakikisha watoto hao hawaachi masomo na kurudi tena mtaani.
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho, wamesema watahakikisha wanafuata maelekezo yaliyotolewa ili kukamilisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wote nchini wanapata elimu kulingana na mahitaji yao.




Discussion about this post