MOSCOW,URUSI
URUSI imeendelea kugonga vichwa mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi duniani kote kutokana na jinsi ilivyozima uasi wa Kundi la Kijeshi la Kampuni binafsi maarufu kama Wagner lililokuwa likiongozwa na Evgeny Prigozhin
Kundi hilo liliamua kuasi na kuandamana kuelekea jiji kubwa kabisa la nchi hiyo la Moscow kutoka nchini Ukraine walikokuwa wakipigana kwa kile walichodai kuupindua uongozi wa kijeshi na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Sergei Shoigu mnamo Juni 24,2023.
Hata hivyo wakati mapigano yakiendelea Wagner waliteka jiji la Rostov-on-Don, Jiji Kuu la Kusini mwa Urusi na kushikilia Kamandi Kuu ya Kijeshi inayoratibu oparesheni ya kijesi nchini Ukraine iliyoanzishwa mnano Februari 24,2022 kwa amri ya Rais wa nchi hiyo Vladmir Putin.
Wakati dunia ikifuatilia tukio hilo ghafla Kiongozi wa Wagner Evgeny Prigozhin alitangaza kuamuru wanajeshi wake warudi kambini na yeye kukubali kwenda uhamishoni nchini Belarus kuepusha mapigano ambayo yangemwaga damu ya Warusi.
Uamuzi huo ulianza kutekelezwa mara moja ambapo misafara ya magari na zana za kijeshi vilianza kuondolewa katika Jiji la Rostov-on-Don hali iliyoruhusu kurudi kwa hali ya kawaida kana kwamba hakukuwa na tukio kubwa masaa kadhaa nyuma na kuacha maswali hasa katika nchi zinazounga mkono upande wa Ukraine ambayo majeshi ya Urusi yanaendelea kupigana katika ardhi ya nchi hiyo.
Licha ya uasi wa kundi la Wagner lakini mapigano yalikuwa yakiendelea katika ardhi ya Ukraine baina vikosi vya Urusi na vile vya Ukraine ambapo wengi walidhani kuwa hiyo ndio ilikuwa nafasi nzuri kwa Ukraine kurudisha maeneo yake yaliyotwaliwa na Urusi.
Tukio la uasi wa Wagner limeonesha kuwa Urusi inaungwa mkono na nchi duniani ambapo baadhi ya nchi hizo zilishindwa kuficha hisia zao na kutamka hadharani kuwa wanamuunga mkono Rais Putin na warusi dhidi ya uasi huo.
Dunia iliendelea kusubiri kitakachotokea lakini badala yake moto huo ulizimika ghafla na vita kuendelea nchini Ukraine kama kawaida licha ya tukio hilo kubwa lilioacha alama kwa Taifa hilo lenye nguvu kubwa za nyuklia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Japan (NHK) katika taarufa yake ya Juni 27,2023 lilimnukuu Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya,( EU) Josep Borrell akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za EU nchini Luxembourg Juni 26,2023 kubadilishana mitazamo kuhusu athari za uasi uliofanywa mwishoni mwa wiki na kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi ya Wagner.
Borrell amesema hali ya Urusi “imekuwa si ya kutabirika tangu mwanzoni, na inaendelea kutotabirika.”
Ameongeza kuwa wakati nguvu ya Urusi awali ilikuwa tishio, sasa kama nchi yenye nguvu kubwa ya nyuklia imekuwa “hatari kwa sababu ya kuyumba kwa siasa za ndani na udhaifu.”
Borrell amesema kwamba EU itaongeza kila aina ya msaada kwa Ukraine, hususani wa kijeshi.
Mawaziri hao wa mambo ya nje wamekubaliana kuongeza kikomo cha juu cha jumla cha fedha inayotumika kwa ajili ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine kwa yuro bilioni 3.5 au takriban dola bilioni 3.8.




Discussion about this post