NA MWANDISHI WETU
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amependekeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mfumo madhubuti wa kudhibiti na kusimamia Pembe za Ndovu.
Mbali na hilo lakini pia Wizara iande mfumo madhubuti wa kuhifadhi kumbukumbu za taarifa zote zinazohusiana na Pembe za Ndovu, ukiwamo mpango mkakati wa taarifa za upotevu kutokana na matukio yasiyotarajiwa kama vile moto.
Mapendekezo hayo ameyatoa katika Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyoitoa Machi 29, 2023 kuhusu Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2022
Amesema wakati wa ukaguzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, amebaini kuwa Mei 16, 2022, Katibu Mkuu wa Wizara aliunda timu ya uhakiki mali ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka Mamlaka ya Usimaizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), DW, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA), na Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Amesema timu hiyo iliundwa kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuhesabu na kupima akiba ya nyara katika ghala la Dar es Salaam.
“Nilibaini kasoro zifuatazo,kutopatikana kwa taarifa sahihi za pembe za ndovu zilizohifadhiwa, kwa ajili ya kufanya tathmini, na kuzipima upya pembe hizo za ndovu;Hali isiyoridhisha ya pembe zote zilizohifadhiwa kiasi cha kusababisha kuharibika kwa ubora na hadhi yake.
“Kushindwa kuhuisha rejista juu ya hali na thamani za pembe za ndovu,programu iliyotumika kurekodi na kusajili akiba ya pembe za ndovuna nyara zingine kutounganishwa na seva kuu ya programu ya Wizara kwa sababu programu hiyo ilikuwa imepitwa na wakati.
“Baadhi ya pembe za ndovu zilikosa taarifa zake za maandishi, huku nyingine zikiwa na taarifa zisizosomeka kutokana na ubovu wa paa ya kuhifadhia jambo linalopelekea kuvuja kwa paa hilo”amesema CAG Kichere
CAG Kichere ameongeza kuwa amebaini pia zana za kuwekea alama zilizotumiwa kurekodi taarifa juu ya pembe za ndovu ziliandikwa kwa wino unaoweza kufutika, na kuzifanya ziweze kufutika kwa urahisi.
“Ghala la kuhifadhia lilikuwa katika hali mbaya kutokana na kuwa na nafasi ndogo, paa kuvuja, hewa chafu, mazingira machafu, umeme usio imara, ukosefu wa vifaa vya kamera, pamoja na ukosefu wa vifaa vya kuzima moto”amesema CAG Kichere
Hata hivyo CAG Kichere amefafanua kuwa mbali na hayo lakini pia amebaini kuwa mwaka 2013 kulikuwa na moto katika ghala la pembe za ndovu ambao ulisababisha kupotea kwa taarifa muhimu zinazohusiana na pembe za ndovu zilizohifadhiwa.
“Jambo la kushangaza ni kuwa hakuna uchunguzi uliofanyika ili kubaini chanzo cha moto huo na madhara yake hadi wakati wa ukaguzi.
“Kwa maoni yangu, ukosefu wa udhibiti sahihi wa Pembe za Ndovu unaweza kusababisha upotevu wa taarifa zinazohusiana na pembe za ndovu.
“Taarifa hii ni muhimu katika kesi za kisheria dhidi ya ujangili na juhudi nyingine zinazolenga kudhibiti vitendo vya ujangili”ameeleza CAG.Kichere
Aidha amebainisha kuwa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii imethibitisha kuwepo kwa mapungufu hayo na itafanya uhakiki wa nyara kila baada ya miaka mitatu hadi minne, kulingana na upatikanaji wa rasilimali.




Discussion about this post