NA GOODLUCK HONGO
WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam nchini Tanzania wameshangazwa na Kaburi la ajabu ambalo limeshindwa kuhamishwa huku likizungukwa na majengo marefu.
Kaburi hilo lililopo eneo la Posta katikati ya Jiji la Dar es salaam (maarufu kama Kaburi moja) linadiwa kuwepo eneo hilo kwa zaidi ya miaka 70 iliyopita huku kukiwa na maelezo yanayochanganya kuhusu uwepo wake.
Hata hivyo Bajeti Communication ilimtafuta Afisa Habari wa Jiji la Dar es Salaam Tabu Shaibu kuelezea uwepo wa Kaburi hilo na sababu za kushindwa kuhamishwa katika eneo la bustani ya watu kupumzika.
Akizungumzia Kaburi hilo Shaibu alikiri kulifahamu na kueleza kuwa ni Kaburi la Sharifu “Nalifahamu ni Kaburi la Sharifu lakini kuna mhusika ambaye ni Afisa Utamaduni ndiye atakayekupa maelezo zaidi juu ya kaburi hilo”amesema Shaibu
Mmoja wa mafundi viatu katika eneo la Posta Saidi Mohamed amesema yeye analijua Kaburi hilo tangu miaka ya 1980 akiwa kijana mdogo na hajui ni kwa nini limeshindwa kuondolewa.
“Ndilo Kaburi pekee katikati ya Jiji la Dar es Salaam na eneo lililopo ndipo watu wengi hukutana kama sehemu ya kijiwe maarufu kama ‘Kaburi Moja’ na eneo hilo miaka ya nyuma ndipo watu maarufu walikuwa wakikutana na kupanga mipango yao wakiwemo wanamuziki wa bendi mbalimbali za zamani “amesema Mohamed
Mohamed ameongeza kuwa katika jiji la Dar es Salaam kulikuwa na maeneo makubwa matatu ambayo watu maarufu walikuwa wakikutana kwa kuwa simu hazikuwa nyingi kama ilivyo sasa ambapo eneo la kwanza ambalo ukimtafuta mtu utampata yalikuwa ni Posta,Kaburi Moja na Mnazi Mmoja ndio maaeneo maarufu kwa watu kukutana miaka ya nyuma na mipango yote hupangwa katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Aisha Seleman ambaye hukaa eneo hilo kusubiri kupata kazi amesema yeye awali alikuwa hajawahi kuliona Kaburi hilo lakini aliavyoanza kukaa hapo ndipo alipoliona na kushangaa kuwa katika eneo lenye pilikapili nyingi.
“Ninavyojua nasikia hili lilikuwa eneo la Msikiti sasa wakasema haiwezekani kujenga Msikini na Kaburi pembeni,waamue ujengwe Msikiti na Kaburi lihamishwe lakini kila walivyotaka kulihamisha ilishindikana,nasikia wamefanya kila linalowezekana kulihamisha imeshindikana ndio wakaamua kuliacha hadi sasa na Msikiti haukujengwa tena”amesema Seleman
Hata hivyo Seleman amebainisha kuwa kwa taarifa alizopata yeye ni kwamba vifaa vilivyotumika kuchimba ili kuliondoa Kaburi hilo vilivunjika vunjika huku wengine wakisema walipotaka kulihamisha walitoka nyuki.
Aidha Seleman ameongeza kuwa baadhi ya watu hufika katika eneo hilo kuomba dua mbalimbali ,“ni eneo ambalo watu mbalimbali hufika wakiamini kuwa matatizo yao yataondolewa baada ya kuomba”amesema Seleman
Uchunguzi wa Bajeti Communication umegundua kuwa eneo lililo Kaburi hilo ni takribani hatua moja tu kilipo kituo cha tax ambapo magari mengine hupaki jirani na kaburi hilo huku viti vilivyojengwa kwa saruji vikizunguka bustani hiyo ya Kaburi Moja.
Bajeti Communication inaendelea kufuatilia zaidi kujua sababu za kutohamishwa kwa Kaburi hilo ndani ya eneo la bustani ambapo makumi ya watu hukaa eneo hilo kusubiri kazi na wengine kufanya biashara.




Discussion about this post