NA MWANDISHI WETU
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania (CAG) Charles Kichere amesema suala la wafungwa kurudishwa tena magerezani bado ni changamoto,baada ya kubainisha wahalifu 3,252 walioachiwa huru kurudishwa tena gerezani.
Amesema suala hilo huenda linachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa fursa za ajira pamoja na unyanyapaa katika jamii unaowakabili wafungwa walioachiwa huru.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya CAG Kichere aliyoitoa Machi 29, 2023 kuhusu Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2022 amesema alipitia Ripoti ya Magereza ya mwaka 2021/22 na kubainisha kuwa wafungwa 3,252 wamerudishwa gerezani tena katika kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema wafungwa 2,320 wamerudishwa gerezani tena kwa mara ya pili na wafungwa 932 wamerudishwa gerezani tena kwa mara ya tatu na kuongeza kuwa kiwango kisichoridhisha cha kuwabadilisha tabia wafungwa wakati wa kifungo chao kinaweza kuwa sababu kubwa inayochangia hali hii.
“Hii inamaanisha kuwepo kwa gharama kubwa za kuwatunza wafungwa hawa jambo linaloiweka Serikali katika matumizi makubwa ya rasilimali.
“Wahalifu walioingizwa upya magerezani na kufungwa jela mara ya pili ni wanaume 2,261,wanawake 46,vijana chini ya miaka 14 ni 13 jumla ni 2320,hukumu ya kifungo kwa mara ya tatu wanaume ni 924,wanawake wanne na vijana chini ya miaka 14 ni wanne na jumla ni 932 na jumla ya wote wanaume ni 3185,wanawake 50 na vijana chini ya miaka 14 ni 17 na jumla ya idadi ni 3252”amesema CAG Kichere
CAG Kichere amebainisha kuwa Menejimenti ilieleza kuwa inajitahidi kufanya mageuzi makubwa katika mipango ya urekebishaji, na wameandaa na kuwasilisha rasimu ya marekebisho kwa mamlaka za juu.
Aidha ameeleza kuwa kwa sasa wanatoa mwongozo na mafunzo kuhusu programu za kuwarekebisha tabia, kutumia rasilimali zilizopo ndani ya huduma hiyo, na kufanya shughuli mbalimbali kama vile viwanda vidogovidogo, Kilimo, Ufugaji, Ujenzi, Uvuvi na mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha Ruanda mkoani Mbeya kwa wafungwa wote waliotiwa hatiani.
“Ninapendekeza menejimenti ya Idara ya Jeshi la Magereza kuimarisha utaratibu wa kurekebisha tabia na kuanzisha mipango ya motisha ambayo inaweza kuwa njia bora za kushughulikia tatizo la kurudia vifungo.
“Programu za kurekebisha tabia zinapaswa kuzingatia ujuzi wa ufundi pamoja na kushughulikia sababu za msingi za tabia ya uhalifu kwa wafungwa, kama vile uraibu wa dawa za kulevya au afya ya akili.
“Mipango ya kuwapa motisha wafungwa inaweza kuwahamasisha kushiriki katika mipango ya urekebishaji wa tabia na kuwapa msaada wanaohitaji ili waweze kufanikiwa kuingia tena katika jamii”amesema CAG Kichere




Discussion about this post