NA GOODLUCK HONGO
TANZANIA haiwezi kulinganishwa na nchi yoyote duniani kutokana na misingi imara iliyoundwa ikiwemo kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa,Mgambo na Muungano.
Hiyo ni baadhi ya misingi imara iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye aliona mbali kuliko vijana wengine wanaozungumzia kuvunja Muungano.
Hayo yameelezwa na Balozi Mstaafu wa Tanzania nchini Sweden Dkt.Willibrod Slaa Julai 19,2023 nyumbani kwake jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa habari wa Bajeti Communication.
Balozi Dkt Slaa amesema watu wengi hasa vijana hawajui historia ya kuasisiwa kwa misingi imara ya Taifa hili ambapo hujiunga na siasa za hamasa wakitaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uvunjwe.
Balozi Dkt.Slaa ambaye ameiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Ukraine and Lithuania amesema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliona mbali kabla ya kuasisi na kukubali kuanzishwa kwa mambo muhimu ikiwemo Muungano,Jeshi la Kujenga Taifa na Mgambo.
Akizungumzia kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndio umeunda Tanzania amesema bila Muungano Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume asingekuwa salama.
Amesema Tanzania ilikuwa na maadui wengi kutokana na harakati za kusaidia Uhuru katika nchi nyingi za Afrika hivyo bila Muungano hali ingekuwa hatari leo hii.
“Sisi Mwalimu aliona hilo mapema sana,wakati nikiwa Baraza la Maaskofu,(Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)),Mwalimu alitaka kutembelea taasisi za Kanisa na mara nyingi alikuwa ananiita saa nane usiku ili niweze kumpa dondoo za eneo analokwenda.
“Licha ya kumuandikia na wakati mwingine tunaandika kama hotuba lakini hata siku moja huwezi kusikia amesoma ulichoandika wewe na hali hiyo alikuwanayo Kardinali Rugambwa,sasa siku moja ananiambia Padri,Katibu Mkuu kuna watu wanamdomo mrefu sana wanataka kuvunja Muungano (wakati ule wa G-55).
“Akasema “Kama niko hai sitakubali muungano huu uvunjike na yeyote hata baada ya kifo changu atakayevunja nitamuapiza,nitamuapiza”amesema Dk Slaa
Amesema hakuna Kiongozi yeyote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) atakayekubali kuuvunja Muungano licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto.
Amebainisha kuwa hatukuwa wajinga kusaini mkataba wa Muungano ndani ya masaa kwani hata alama za Marekani ziko mpaka leo Zanzibar lakini vijana wanasema kirahisi kuvunja Muungano kupitia siasa za hamasa.
Amefafanua kuwa watu wengi hawana misingi na ndio wanaojitokeza kutaka kuuvunja Muungano lakini hawajui umuhimu wa suala hilo na misingi yake ya kuanzishwa.
Hata hivyo ameeleza kuwa hakuna Katiba iliyounda Muungano lakini Mwalimu alitoa Dikrii yaani Hati juu ya Muungano ambapo alitoa barua inayoeleza kinachojulikana kama Tanganyika na itaitwa Tanzania ambapo Kiti cha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa kiliondolewa na kikabakia cha Tanzania.
“Ili nchi itambuliwe Umoja wa Mataifa lazima iwe na Kiti Umoja wa Mataifa kama hakuna kiti haiwezi kutambuliwa.
“Wazanzibar wana haki kweli ya kulalamika kwa kupoteza utambulisho wao baada ya muungano lakini wapelekwa polepole bila kuvuragana na ikiwa tutakuja kuvurugana kitachotokea ni hatari”ameonya Balozi Dkt.Slaa
Hata hivyo ameongeza kuwa Wazanzibar wanachoumia ni kwamba hawatambuliwi kwa kueleza kuwa wamepoteza utambulisho na kiti Umoja wa Mataifa .
Amesema ni lazima suala hilo lifanywe kwa utaratibu kwani Mwalimu kama asingeingilia Zanzibar Rais Karume asingekuwa salama na wala sio waarabu ndio wangeshughulika lakini Tanzania ilikuwa ndio adui mkubwa wa makaburu na wareno kutoka Msumbuji.
Amesema makaburu walikuwa ndio wanatawala karibu nchi nyingi za Kusini mwa Afrika na Tanzania ndio ilikuwa ikisaidia nchi hizo kupata uhuru.
“Sisi tulimfukuza Mreno pale Msumbiji na Kaburu alikuwa ndio aliyekuwa na silala akishindana na Ulaya na alitawala karibu kusini kote mwa Afrika sasa kwa Zanzibar ilikuwa ni dakika tano tu kuingia kwa kuleta meli yake moja tu.
“Sheria za kimataifa zinasema nikikuvamia nikakupiga basi maeneo hayo ni ya kwangu na inabadilisha mipaka na kama makaburu wangefanikiwa kupiga basi eneo hilo lingekuwa la kwao na ndio kinachofanywa na Rais wa Urusi Vladmir Putin”amesema Balozi Dkt. Slaa
Akizungumzia kuhusu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) amesema watu wengi na vijana hawajui thamani ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Tanzania na kwa Ukombozi wa Bara la Afrika lakini wao wanajua.
Amesema tangazo la kuanzishwa kwa JKT lilipotolewa kwa vijana kupelekwa huko walipiga kelele yakiwemo madhehebu ya dini juu ya uamuzi huo wa kuchukua watoto wao kupelekwa jeshini.
Amesema watoto wa kike na wa kiume wote hukaa pamoja ndani ya handaki na kelele zilizopigwa ni juu ya maadili ya kuwaweka pamoja vijana wa kike na kiume kwa kuwa hali ya binadamu inajulikana.
Ameongeza kuwa licha ya kuwa na madhaifu yake JKT lakini vijana waliotoka huko wamekomaa na kujengwa katika utu na kuthamini na kupelekea wengine kuoana wakiwa makabila tofauti na hata kula chakula wasichokijua na kuwafanya kuwa ndugu.
“Sasa hujui unavyojengwa katika utu wako na kudhamini watu wale na ukatapa mchumba kule Mtwara sasa hapo watanzania watapigana kweli? Hivi vitu ni vya Tanzania pekee huwezi kulinganisha na nchi yoyote,na vitu hivi havikuja hivihivi tu bali vimeundwa na kwa misingi hiyo Tanzania haiwezi kupigana vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na mifumo kama na nchi zingine duniani.
“Wakati wa vita na Uganda waliotangulia vitani ni JKT na Jeshi la Akiba (Mgambo) sasa vitu hivi ni lazima vijana waelewe msingi wake wasione vyaelea wajue vimeundwa”amesema Balozi Dkt.Slaa




Discussion about this post