NA GOODLUCK HONGO
PAMOJA na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali dhidi ya kupambana na vitendo vya ujangili katika maeneo mbalimbali ya hifadhi na mapori ya akiba,wanyamapori pia wanakabiliwa na magonjwa mbalimbali yanayotishia uhai wao.
Akizungumza na Bajeti Communication jijini Dar es Salaam,Kamishna Msaidizi kutoka Kanda ya Kusini Mashariki ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Keneth Sanga amesema kuna magonjwa mengi yanayowapata wanyamapori lakini yapo baadhi ambayo yanayojulikana sana.
Amesema wanyamapori wanakabiliwa na Ugonjwa wa Miguu na Midomo (Foot and Mouth Disease) ambapo huo huwapata pia Ng’ombe, mbuzi na kondoo.
“Kichaa cha Mbwa (Rabies), huu ni ugonjwa unaowapata pia jamii ya Mbwa mfano Fisi na Mbwa Mwitu.
“Homa ya Nguruwe (African Swine fever) hii pia inawapata wanyamapori kama Ngiri na Nguruwe pori.
“Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) huu huwapata Wanyamapori jamii ya Ngo’mbe kama Nyati”amesema Kamishna Msaidizi Sanga
Kamishna Msaidizi Sanga ameongeza kuwa hayo ni magonjwa machache tu yanayowapata wanyamapori licha ya kuwa yapo mengi.
Hata hivyo kutokana na uvamizi wa njia za wanyamapori zinazowasaidia kuhama kutoka hifadhi moja hadi nyingine maarufu kama (Shoroba) kwa ajili ya kuzaliana na kutafuta malisho upo uwezekano wa magonjwa hayo kuwapata binadamu kutokana na makundi ya wanyama hao kuingia na kuweka kambi katika makazi ya watu.
Aidha mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha mafuriko na ukame hupelekea wanyamapori kuvamia makazi ya watu ili kutafuta chakula na maji hali ambayo pia inaweza kusambaza magonjwa hayo kwa binadamu na mifugo wanayoifuga.




Discussion about this post