NA MWANDISHI WETU,DODOMA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahaman Kinana,amesema kutokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Taifa, watu waliojaribu kuigawa nchi kwa misingi ya udini ,ukabila,ubara na visiwani wameshindwa.
Hata hivyo amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka miwili ya uongozi wake yanatokana na utulivu, usikivu, kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania.
Kinana ameyasema hayo leo Julai 23, 2023 alipokuwa qkiwahutubia wananchi wa Kondoa mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Dk. Ashatu Kijaji kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2023.
Amesema kuna watu wamejaribu kuwagawa kwa misingi ya ukabila wameshindwa, na kuna watu wamejaribu kuwagawa kwa misingi ya ubara na visiwani wameshindwa pia.
“Kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ukabila wameshindwa, kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ubara na visiwani wameshindwa,” amesema Kinana
Amebainisha kuwa kwa hali ilivyo na kwa hatua waliyopiga mpaka kufika 2025 ana uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema waendelee na CCM pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM lakini tunaangalia na wenzetu wa nchi jirani wanakwendaje, Nchi yetu imetulia, inamaani, ina umoja, inamshikamano na malengo, na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina Ilani nzuri inayotekelezeka,” amesema Kinana.

Wakati huo huo Kinana, amewashauri viongozi wa CCM hicho katika ngazi zote kuendeleza umoja ili kwenda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 wakiwa wamoja ili kuibuka washindi.
Kinana ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa CCM katika kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
“Napongeza kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa CCM hususan katika ngazi kitongoji, Kijiji, mtaa na Kata kwa kazi nzuri mnayoifanya na mwakani ni mwaka wa uchaguzi, hivyo naamini wana CCM tutakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka 2024 tukiwa kitu kimoja, tukifanya kampeni wamoja na tutaibuka na ushindi tukiwa wamoja, hivyo hivyo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025,” amesema Kinana.
Kinana amewasili mkoani Dodoma kuanza ziara katika mikoa ya Manyara, Mara, Simiyu na Tabora




Discussion about this post