NA MWANDISHI WETU
UKAGUZI uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere umebaini kuwa jumla ya milipuko 1,718 ya moto iliyotokea katika mikoa 28 ya zimamoto kwa mwaka 2021/22 haijachunguzwa.
Kifungu cha 5(2c) cha Sheria ya Zimamoto na Uokoaji Na. 14, 2007 kinaipa mamlaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF) kufanya ukaguzi wa moto ili kupata taarifa zinazohusiana na chanzo cha moto na hasara iliyosababishwa na moto.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania (CAG) Charles Kichere aliyoitoa Machi 29, 2023 kuhusu Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2022
Amesema imebainika kuwa hakuna tukio lolote kati ya matukio hayo ya moto lililochunguzwa, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 5(2c) cha Sheria ya Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya mwaka 2007.
Aidha, amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21, kati ya milipuko 1,967 ya moto iliyorekodiwa, ni matukio 560 tu yaliyochunguzwa na kusababisha matukio 1,407 ya moto sawa na asilimia 72 kutokuchunguzwa.
“Kwa matokeo haya ukosefu wa uchunguzi unaweza kuzuia uwajibikaji na kuathiri juhudi zinazolenga kuzuia matukio ya moto kwa baadaye.
“Matukio ya mlipuko wa moto na ripoti ya uchunguzi kutofanya uchunguzi wa moto kumesababishwa na uhaba wa watumishi.
“Hii inamaanisha kuwa, sababu za moto hazifahamiki, jambo ambalo linaweza kusababisha ukosefu wa hatua za kuzuia moto na uwezekano wa matukio ya moto kujirudia”amesema CAG Kichere
CAG Kichere amebainisha kuwa kulingana na matokeo ya ukaguzi, anashauri mamlaka husika zichukue hatua kwa kuhakikisha kufuata Kifungu cha 5(2c) cha Sheria ya Zimamoto na Uokoaji Na. 14 ya mwaka 2007, kwa kufanya uchunguzi wa milipuko na matukio yote ya moto yanayotokea ndani ya mikoa ya Zimamoto.
“Kuandaa na kutekeleza mfumo wa kuchunguza matukio ya moto ambayo ni pamoja na miongozo na itifaki za kubaini chanzo cha matukio ya moto na kuchukua hatua stahiki za kurekebisha.
“Kuongeza fedha kwa ajili ya shughuli za uchunguzi wa moto ili kuwezesha mafunzo kwa wachunguzi, ununuzi wa vifaa muhimu,na kuboresha mchakato wa uchunguzi kwa ujumla.
“Kuimarisha uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kutoa taarifa za matukio ya moto mara moja na kwa usahihi ili kuboresha ubora wa taarifa zilizopo kwa ajili ya uchunguzi”amesema CAG Kichere




Discussion about this post