NA MIRIAM SARAKIKYA, ARUSHA
SERIKALI imetoa zaidi ya tani 40,685 za mbolea ya ruzuku kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha Arusha,Kilimanjaro na Manyara ambapo zaidi ya wakulima 89,300 wamenufaika.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zuberi Ali Maulidi wakati akifungua maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika Viwanja vya Njiro jijini Arusha
Amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23 Serikali ya Tanzania iliweka nguvu kubwa katika kuboresha Kilimo,Uvuvi na Mifugo ambapo mikoa ya Kanda ya Kaskazini imenufaika na mambo mbalimbali ikiwemo utolewaji wa mbolea za ruzuku kwa ajili ya kuongeza tija kwenye kilimo.
Aidha ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 jumla ya Tani 17288 zimetolewa kwa Mkoa wa Arusha na kuwanufaisha wakulima 19663 .
Mbali na Mkoa wa Arusha,mikoa mingine iliyopokea mbolea hiyo ya ruzuku ni pamoja na Kilimanjaro tani 18557 na kuwanufaisha wakulima 62829 huku Mkoa wa Manyara ukipata tani 4840 na kuwanufaisha wakulima 6829.
“Tunawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili iweze kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwani maonesho haya yana lengo la kuonyesha fursa zilizopo katika Sekta za Kilimo,Mifugo na Uvuvi na kutoa elimu kwa wakulima,wafugaji na wavuvi ili uzalishaji wa mazao na bidhaa zinazotokana na sekta hizo uwe na tija na hatimaye kuchangia katika ukuwaji wa uchumi wa nchi”amesema Maulidi
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema Maonesho ya Wakulima Nanenane yamezidi kuimarika na kuleta chachu katika sekta mbalimbali hivyo ushirikiano wa kimuungano utaendelea kuleta chachu zaidi kwa wananchi wote wa Tanzania Bara na Visiwani.

Wakati huo huo Kampuni ya Agricom Africa imetambulisha zana mpya za Kilimo zitakazowasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi na kulima kwa kisasa zaidi.
Miongoni mwa zana hizo mpya za Kilimo ni pamoja na trekta aina ya Kubota yenye nguvu(horsepower 75) ambayo inatofautishwa na trekta nyingine zilizopo sokoni.
Akizungumzia zana hizo mpya, Meneja wa Kanda ya Kati na Kaskazini wa Kampuni hiyo Peter Temu,amesema uwezo wa trekta hiyo ni sawa na uwezo wa kutumia trekta mbili kwa mara moja ikiwa na na uwezo wa kufanya kazi mahali popote kulingana na aina ya udongo.
Aidha ameongeza kuwa mategemeo yao ni kuwasaidia wakulima wa Kanda ya Kaskazini kuweza kufanya vizuri kwenye kilimo chao ukitengemea trekta hiyo yenye ubora mkubwa kwenye matumizi ya mafuta ,bei inayouzwa hadi katika upatikanaji wa vipuri
Temu amewataka wakulima kutarajia kupata faida kutokana na kile wanachokifanya huku akisema kuwa teknolojia hiyo ni ya kijapani na inasambazwa na Agricom Afrika pekee ambapo pia hutathimini njia ya kumuwezesha mkulima kuweza kupata faida zaidi kwa kumuinua kutoka katika matumizi ya zana za zamani na kurudi katika matumizi ya zana za kisasa.




Discussion about this post