NA MWANDISHI WETU
MVUA zinazoendelea kunyesha mkoani Dar es Salaam zimeendelea kuathiri miundombinu ya barabara ikiwemo nyumba nyingi kujaa maji na kusababisha baadhi ya maeneo kutofikika baada ya barabara kukatika kutokana na udongo kusombwa na maji.
Uchunguzi uliofanywa na Bajeti Commucation batika maeneo mbalimbali ya huo umegundua kuwa baadhi ya maeneo hasa kutoka barabara kuu zilizojengwa kwa kiwango cha lami zimeathirika vibaya kutokana na maji kujaa katika nyumba na zingine kubomoka kabisa.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 17,2023 jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Stakishari uliopo Kata ya Kipawa Jimbo la Segerea Rehema Nyagorena amesema wao kama Serikali ya Mtaa wanaendelea na jitihada za kuchimba mitaro ili kuondoa maji yaliyojaa katika nyumba nyingi za watu.
“Tunachangamoto kubwa sana juu ya mvua hii,kutokana na mtaa wetu kutojengwa vizuri na tunajaribu kukabiliana na kujaa kwa maji ili yaweze kuondoka katika makazi ya watu lakini pia hadi sasa hatuna vifo katika mtaa wetu vilivyotokana na mvua hii”amesema Nyagorena
Hata hivyo Nyagorena ameongeza kuwa mbali na mvua hiyo kuleta madhara lakini pia wana Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi maarufu kama (DART) ambapo kutokana na ujenzi unaoendelea umesababisha pia mitaro kuziba hivyo kuongeza kujaa kwa maji katika nyumba za watu.
“Tumewaomba watusaidie kuweka hata mabomba ili kuyafanya maji yaweze kusafiri na wao wamekubali hivyo tunatarajia kupungua kwa maji katika barabara za mitaa na nyumba za watu”amesema Nyagorena
Akizungumzia watu kupita ndani ya mtaro wa Reli ya Mwendokasi (SGR),amebainisha kuwa hiyo sio njia rasmi na wamekuwa wakiomba eneo hilo kuwekewa kivuko ili kuzuia watu kupita ndani ya mtaro na kutokea upande wa pili kutokana na eneo hilo kuwekewa uzio wa kuzuia watu kuvuka.
“Tuliongea na uongozi wa Reli na wao walituambia kuwa kivuko kitawekwa kila baada ya kilomita moja hivyo kutoka njia panda ya majumba sita hadi katika karavati hilo ni karibu sana lakini bado tunaimani kuwa muafaka utafikiwa na ikishindikana basi tutawaomba wauzibe ili kuondoa hatari kwa kuwa baadhi ya watu waliwahi kuzimia walipoingia ili wavuke”amesema Nyagorena

Hata hivyo walilazimika kuweka walinzi katika kipindi hiki cha mvua ili wanafunzi na watu wengine wasivuke lakini changamoto kubwa ni kuwa watu wengi wameshazoea kuvuka kwa kuingia ndani ya shimo hilo la kupitishia maji hivyo wamekuwa wagumu kuzunguka na kupita katika njia rasmi zilizowekwa.





Discussion about this post