TEHRAN,IRAN
HALI katika Mashariki ya Kati imeendelea kuwa tete baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kufanya mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel likijibu mashambulizi yaliyofanywa na Israel ya Aprili mosi,2024 dhidi ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo katika Mji Mkuu wa Syria, Damascus.
Mashambulizi hayo yanakuja wakati ambapo Israel inaendelea na vita katika Ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la Hamas vilivyoingia mwezi wa sita tangu Hamas ilipoivamia Israel Oktoba 7,2023 na kuwaua waisrael zaidi ya 1000 na kuwateka nyara wengine zaidi ya 200.
Vyombo vya habari vya Iran vimetangaza kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limefanya mashambulizi usiku wa kuamkia Aprili 15,2024 na kuitaja operesheni hiyo kuwa ni “Operesheni Ahadi ya Kweli.”
Katika mitandao ya kijamii ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali ya Iran vimeonesha jinsi makombora hayo yalivyopiga na kulipuka katika miji ya Israel huku Israel ikikiri kuwa Iran imerusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora katika ardhi za nchi hiyo.
Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani, ameonya kwamba “nchi yoyote ambayo itakayofungua ardhi au anga yake kwa Israel kwa ajili ya kuishambulia Iran, itapata majibu madhubuti.”
Shambulio la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus lilisababisha kuuawa kwa Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi, Kamanda wa Kikosi cha IRGC, Naibu wake, Jenerali Mohammad Hadi Haji Rahimi, na maafisa watano walioandamana nao jambo lililoighadhabisha Iran na kuapa kulipiza kisasi licha ya Marekani na nchi za magharibi kuionya Iran kutothubutu kuishambulia Israel.
IRGC imesisitiza katika taarifa yake kwamba, operesheni hiyo ya kulipiza kisasi imefanyika baada ya kimya na upuuzaji wa siku 10 wa mashirika ya kimataifa, haswa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili kulaani uchokozi wa Israel kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Ushirikiano wa Urusi na Iran,Marekani na Israel
Vita hivyo vinaweza kuchukua sura mpya kutokana na Iran kuwa na ushirikiano wa karibu na Urusi inayoendelea na vita vyake na Ukraine ambapo Marekani na nchi za Magharibi wameapa kuishinda Urusi kwa kuisaidia Ukraine kwa kuipatia misaada ya kijeshi na vifaa vya kisasa hali inayoifanya Urusi kulalamika na kuyaonya mataifa hayo juu ya madhara ya misaada hiyo.
Hata hivyo kitendo cha Marekani na washirika wake kuiunga mkono Ukraine kwa hali na mali kunaweza kuifanya Urusi nayo kuisadia Iran kupambana na Israel na washirika wake ambao ni Marekani na nchi za magharibi zinazoipatia misaada Israel na kuifanya Iran kutoogopa maonyo yote yaliyotolewa na nchi za magharibi akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden kwa Iran kutothubutu kuishambulia Israel.
Kundi la waasi wa Houth wanaungwa mkono na Iran ambao wanatawala nusu ya nchi ya Yemen ilizindua mashumbulizi ya kuziangamiza meli zote zinazohusiana na Marekani,Uingereza na za nchi zingine ambazo zinaelekea Israel ikiwa na lengo la kuifanya Israel kusitisha vita vyake na Hamas vilivyouwa wapalestina zaidi ya 32,000 hadi sasa hali iliyolifanya eneo hilo kuwa tete zaidi.
Uingereza tayari imeonja machungu ya mashambulizi hayo baada ya meli yake kubwa ya kubeba makontena kuzamishwa kutokana na kushambuliwa na makombora ya waasi hao wa Houth.




Discussion about this post