NA MWANDISHI WETU
VITUO binafsi vya kutolea huduma za afya nchini vimetajwa kuongoza katika kuwafanyia upasuaji akina mama wanaokwenda kwa ajili ya kujifungua watoto wao tofauti na vya Serikali.
Hata hivyo asilimia 11 ya watoto waliozaliwa hai ndani ya miaka miwili kabla ya utafiti walizaliwa kwa njia ya upasuaji.
Hali hiyo imetajwa katika Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (DHS-MIS 2022) uliofanywa na na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na taasisi zingine ikiwemo Wizara ya Afya.
Utafiti huo umebainisha kuwa njia ya upasuaji inatumika zaidi katika vituo binafsi kuliko vituo vya umma.
‘’Kiwango kikubwa cha kujifungua kwa njia ya upasuaji kinaonekana zaidi maeneo ya mijini kwa asilimia 19 ikilinganishwa na maeneo ya vijijini ambapo ni asilimia nane.
‘’Njia ya upasuaji inatumika zaidi katika vituo binafsi kwa asilimia 30 kuliko vituo vya umma kwa asilimia 12.”umebaini utafiti huo
Mbali na hilo lakini pia utafiti huo umefafanua kuwa kujifungua kwa upasuaji kunaongezeka kadri hali ya uchumi wa kaya inavyoongezeka kutoka kiwango cha chini cha asilimia nne hadi kiwango cha juu cha asilimia 24.
Kwa upande wa huduma za kujifungua,utafiti huo umebainisha kuwa asilimia 81 ya watoto hai walizaliwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, kiasi kikubwa cha watoto ambacho ni asilimia 75 walizaliwa katika vituo vya umma.
‘’Bado ipo changamoto ya watoto wanaozaliwa majumbani ambapo Utafiti huu unaonesha kuwa asilimia 18 ya watoto walizaliwa nyumbani’’umeongeza utafiti huo
Hata hivyo utafiti huo umeonesha kuwa, kwa ujumla kiwango cha akina mama wanaojifungulia vituo vya kutolewa huduma za afya kimeongezeka katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita kutoka asilimia 52 hadi asilimia 81 na asilimia ya watoto wanaozaliwa nyumbani imepungua kutoka asilimia 47 hadi asilimia 18.
Awali akizungumzia utafiti huo wakati wa semina ya waandishi wa habari kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) Mtakwimu Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Elinzuu Nikodem amesema Utafiti huo umefanyika nchi nzima ikiwemo na Zanzibar.
Amesema Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (DHS-MIS 2022) ulilenga kutoa takwimu za kufuatilia na kutathmini hali ya afya ya watu nchini Tanzania.
Amesema Utafiti wa DHS-MIS wa Mwaka 2022 ni wa saba katika mfululizo wa tafiti za kitaifa za kidemografia na afya zilizowahi kufanyika nchini Tanzania tangu mwaka 1991-92.
‘’Lengo la Utafiti huu ni kupata taarifa muhimu kuhusu kiwango cha uzazi, ndoa, kujamiiana, upendeleo wa kuzaa, ufahamu na matumizi ya njia za uzazi wa mpango, unyonyeshaji watoto wadogo, lishe, vifo vya watoto wadogo na vifo vitokanavyo na uzazi,
‘’ Huduma wakati wa ujauzito na huduma za watoto, malaria, na taarifa nyingine zinazohusu afya, pamoja na kiwango cha malaria kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano’’amesema Nikodem




Discussion about this post