NA MWANDISHIN WETU
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limefanikiwa kuandika historia mpya kwa kununua ardhi na majengo katika eneo la Urafiki, mkoani Dar es Salaam, ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania-China Friendship Textile Mills Co.
NHC ilinunua ardhi na majengo katika eneo hilo la Urafiiki baada ya mnada uliofanyika Novemba 3, 2023, uliondeshwa na Kampuni ya Udalali ya Santana Investment Limited na kufanikisha upatikanaji wa ekari 105 za ardhi katika viwanja vitatu vya kimkakati mkoani Dar es Salaam.
Viwanja hivyo ni pamoja na Kiwanja Namba 2010, Kitalu ‘D’, Sinza chenye ukubwa wa ekari 58, Kiwanja Namba 1, Kitalu ‘48’, Ubungo Industrial Area chenye ekari 8.42, na Kiwanja Namba 2, Kitalu ‘48’, Ubungo Industrial Area chenye ekari 39.5 ambapo ununuzi huo muhimu unaimarisha dhamira ya NHC ya kuendeleza maeneo yenye thamani na kukuza uchumi wa taifa.
Licha ya uwepo wa unit 399 kwa ajili ya makazi pia kuna majengo ya biashara sita, makazi ya wataalamu 32, Shule ya msingi, retail shop 32, maghala 31, yadi za magari 10, gereji 4, kituo cha mafuta 1, sehemu za kuosha magari tatu, fremu ndogo ndogo, makontena na Industrial park.
NHC imejipatia sifa nzuri miongoni mwa Watanzania kutokana na ubunifu wake, utekelezaji, na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa nyumba bora za makazi na biashara.
Hatua za Awali na Matayarisho
Baada ya kufanikisha ununuzi wa ardhi hiyo, NHC iliingia kazini mara moja kwa kutekeleza majukumu muhimu ikiwemo kufanya utambuzi wa maeneo yote yaliyopatikana na kuanza mchakato wa upangishaji upya wa majengo yaliyopo.
Aidha, NHC ilianza taratibu za kupata hati miliki kutoka Wizara ya Ardhi kwa ajili ya eneo la Urafiki, huku ikifanya ukaguzi wa wapangaji na kutoa mikataba mipya ya upangaji kwa wateja 473. Hatua hizi za awali zimejenga msingi imara wa kuendeleza eneo hili na kuhakikisha mali za NHC zinatumika kwa ufanisi mkubwa.
Katika juhudi zake za kuendeleza maeneo mbalimbali, Mei 17, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alitembelea miradi inayotekelezwa na Shirika hilo mkoani Dar es Salaam.
Ziara hiyo ilimfikisha katika eneo la Urafiki, ambapo wakazi walionyesha furaha na matumaini baada ya kusikia habari za kukamilika kwa ununuzi wa eneo hilo.
Katika mazungumzo yake na wakazi wa Urafiki, Abdallah aliwahakikishia kuwa shirika analoliongoza limedhamiria kufanya mageuzi makubwa kwa kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa na lenye tija.
Aliweka wazi kuwa NHC ina malengo makubwa ya kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa zaidi, likiwa na miundombinu bora na fursa nyingi za kiuchumi.
Changamoto
Pamoja na hatua hizi, NHC ilikumbana na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa shughuli zake eneo la Urafiki. Mojawapo ya changamoto hizo ni uwepo wa wafanyakazi wa zamani wa Kampuni ya Urafiki, ambao walikuwa na madai mbalimbali, ikiwemo masuala ya ajira.
Mbali na hayo lakini pia, mikataba ya upangaji iliyokuwepo kabla ya ununuzi wa eneo hili ilileta ugumu katika upangaji upya wa majengo,hali mbaya ya miundombinu, ikiwemo mifumo ya maji taka, majengo chakavu, na mazingira duni.
Hali hiyo pia ilihusisha uwepo wa wapangaji wasio rasmi, maarufu kama wapangaji hewa, ambao walikuwa wakitumia majengo hayo bila mikataba halali.

Mikakati ya Uendelezaji
Ili kukabiliana na changamoto hizo na kuleta mageuzi makubwa katika eneo la Urafiki, NHC imepanga mikakati madhubuti kwa kuanzisha Mkoa wa Urafiki kwa ajili ya usimamizi wa mali zake mwezi huu wa Agosti 2024. Mkoa huo utahakikisha usimamizi bora na wa karibu zaidi wa ardhi na majengo yote yaliyopo katika eneo hilo.
NHC pia imejipanga kukamilisha mchakato wa upangishaji wa nyumba na maeneo ya biashara ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Agosti 2024 ambapo hatua hiyo itahusisha kutoa mikataba mipya ya upangaji na kuhakikisha kuwa mali za NHC zinatumika kwa manufaa ya shirika na jamii kwa ujumla.
Mbali na hilo lakini pia NHC imepanga kuanza ukarabati na matengenezo ya majengo na miundombinu katika eneo la Urafiki na hapo itahusisha kuboresha mifumo ya maji taka, ukarabati wa majengo chakavu, na kuboresha mazingira ya eneo hilo ili kufikia viwango vya kisasa.
Hata hivyo, NHC imepanga kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa mpango mkakati wa Uendelezaji wa eneo la Urafiki kabla ya Desemba 2024. Mpango huo utaweka dira ya maendeleo ya eneo hilo kwa miaka ijayo, ukilenga kuboresha thamani ya ardhi na majengo ya NHC huku ukichangia ukuaji wa Uchumi wa Taifa.
Kupitia mikakati hiyo, NHC inalenga kuleta mageuzi makubwa katika eneo la Urafiki na kuhakikisha kuwa mali zake zinatumika kwa ufanisi na manufaa kwa jamii. Mafanikio haya ya awali yanaonyesha dhamira ya NHC ya kuwa kinara katika kuendeleza Sekta ya Nyumba na Miundombinu nchini Tanzania.
Kwa kuzingatia mipango yake ya maendeleo, NHC iko njiani kugeuza eneo la Urafiki kuwa kitovu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, likichangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi wa taifa
Uwekezaji huo utalenga kuboresha miundombinu, kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara, na kuanzisha vituo vya huduma mbalimbali ikiwemo matumizi ya teknolojia na kituo cha kutoa na kupokea taarifa kwa lengo la kuboresha huduma zao.
Kituo hicho kitafanya kazi saa 24, hivyo kurahisisha mawasiliano na huduma kwa wananchi. Hatua hii inatarajiwa kuleta ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wakati.
Kwa uwekezaji huu, NHC inaonekana kujipanga kuleta mageuzi makubwa katika eneo la Urafiki, hivyo kuongeza thamani ya eneo hilo na kuboresha maisha ya wakazi wake kwa kiwango kikubwa ikiwemo kuleta maendeleo makubwa,siyo tu katika eneo hilo, bali pia katika uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Matarajio ya Wakazi wa Urafiki.

Wakizungumzia juu ya ufanisi wa NHC, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanaotarajia kunufaika na ujio wa shirika hilo wamesema wanaamini kilio chao cha muda mrefu cha kutaka makazi bora na maeneo ya kufanyia biashara kimepata suluhisho.
Hemed Salum almesema anaamini kuwa mbali ya kuwa na mandhari nzuri, atalipwa stahiki zake alizokuwa akikidai kiwanda cha Urafiki baada ya mauziano hayo ya eneo hilo.
“Nimesikia faraja sana niliposoma na kuona walionunua eneo hili ni NHC,hawa jamaa wana historia nzuri ya kujenga majengo na kutoza kodi inayolipika na tumeona nyumba walizojenga Kawe, Chang’ombe, Kigamboni na kwingineko,” anabainisha Salum
Kwa upande wake Sakina Mambo, mkazi wa Urafiki, amesema majengo anayoyaona kwenye maeneo mengine kupitia vyombo vya habari sasa yanaweza kuonekana katika eneo lake na ikiwezekana yeye kuishi akipewa fursa.
”NHC pia wanasifika kwa kuwatua wananchi mzigo wa malipo ya kodi kwa kuwapa fursa ya kulipa kwa namna wanavyoweza kulingana na kipato chao.
”Mpangaji anaweza kulipa kodi kuanzia mwezi mmoja mmoja tofauti na wenye nyumba wengi ambao wanataka mpangaji alipe miezi sita au mwaka mmoja kwa mara moja”ameongeza Mambo
Halima Shekimweri, mkazi wa Ilala Boma jijini Dar es Salaam, amebainisha kuwa NHC imekuwa mkombozi mkubwa kwao kwa sasa wanalipa kodi nafuu na kwa muda ambao muhusika huamua kulingana na uwezo wake.
“Hizi nyumba za NHC ni kama vile zetu. Tunaweza kulipa kadri ya uwezo wako, ukiamua mwezi mmoja mmoja, miezi sita au mwaka mmoja, ni wewe tu.
Nyumba yenye vyumba viwili, choo, sehemu ya chakula na jiko unalipa 290,000 Kule mtaani nyumba kama hii unaipata kati ya shilingi 400,000 na 500,000”anasema Shekimweri
Zebedayo Juma, mkazi wa Chang’ombe, amesema baada ya kupata nyumba ya NHC hana tena hofu ya kodi na muda wa kulipa kwa kuwa nyumba anayokaa ni ya kisasa ikiwa na vyumba viwili vya kulala, choo, jiko, sehemu ya chakula na analipa Sh.350,000 kwa mwezi.
“Ukweli, nyumba ninayoishi na kwa eneo la hapa ingekuwa mtaani ningelipa zaidi ya Sh. 500,000, tena wangenitaka nilipe kwa mwaka. Lakini NHC wananitoza kwa mwezi, jambo ambalo limenipa unafuu mkubwa wa kujiendeleza kimaisha,” anasema Juma
Joyce Shayo, mfanyabiashara katika eneo la Shekilango, ameeleza kuwa sehemu ya biashara ambayo angelipia zaidi ya Sh. 1,000,000 kwa NHC haizidi Sh.700,000, tena anaweza kulipa kila mwezi.
Amesema hata akikwama, anaweza kufanya nao mazungumzo na kulipa bila kudhalilishwa kwa kufukuzwa au kutolewa maneno ya maudhi.
“Ukweli, kama NHC wangekuwa na uwezo wangejenga kwenye maeneo mengi zaidi ili kuwapa unafuu wa maisha wananchi”anasema Shayo
Samuel Nyarobi anasema kuwa tatizo bado nyumba na majengo ya biashara ni machache na hayakidhi mahitaji ya wananchi,”
”Kwa maeneo ya mijini hivi sasa, chumba chenye choo ndani kinatozwa kati ya shilingi 100,000 hadi 150,000.lakini NHC gharama hiyo unapata nyumba nzuri hasa zile za zamani.
“Namuomba Rais Samia Suluhu Hassan awaongezee mtaji NHC wajenge nyumba nyingi zaidi kwa kuwa mahitaji ni makubwa hasa kutokana na gharama za nyumba na fremu za biashara kuwa kubwa na kulipa kwa mwaka au miezi sita,”anasisitiza Nyarobi.

*Ombi la Kuongezewa Mtaji kwa NHC*
Wakazi wengi wanaamini kuwa kama Serikali itaongeza nguvu kuliwezesha NHC kujenga nyumba za ghorofa nyingi kwa ajili ya kupangisha, itawasaidia wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini wasiomudu kulipa kwa miezi sita au mwaka.
Ombi la kutaka NHC iongezewe mtaji ili lipanue zaidi huduma zake liliwahi kutolewa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ilipofanya ziara katika miradi ya shirika hilo.
PIC ilieleza kuwa linaamini kama NHC watapatiwa fedha zaidi, wataziwekeza katika miliki zenye faida ambapo pia serikali itanufaika kwa kupata kodi.
Kaulimbiu ya NHC ni “Tunalijenga Taifa” imeendelea kuongoza NHC si kwa maneno tu bali kwa vitendo, ambapo kila kukicha miji inabadilika kimwonekano kutokana na majengo mazuri yanayojengwa na shirika hili.




Discussion about this post