BUDAPEST,HUNGARY
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amefanya mazungumzo na Rais wa Hungary, Tamas Sulyok na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano na amani duniani.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Oktoba 8, 2024 katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo Jijini Budapest walijadili njia bora za kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa haya mawili, Tanzania na Hungary, katika sekta mbalimbali hususani Kilimo, Utalii, Biashara na Maji.
Rais Sulyok alitumia fursa hiyo kumpongeza Dkt. Tulia kwa juhudi zake za dhati katika kuendeleza amani duniani, hususani katika maeneo yanayokumbwa na migogoro mikubwa.
Aidha, walizungumzia pia masuala yanayohusu misingi na malengo ya IPU, ambapo Rais Sulyok aliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza ajenda zote za IPU.
Ifahamike kuwa kati ya nchi nane zilizounga mkono kuanzishwa kwa IPU katika mkutano uliofanyika Juni 29 na 30,1889 nchini Ufaransa, Hungary ilikuwa miongoni mwao, sambamba na Uingereza, Ufaransa, Marekani, Denmark, Ubelgiji, Uhispania na Liberia kutoka Afrika.
Hii ndio sababu Hungary inaadhimisha miaka 135 ya kuanzishwa kwa IPU.




Discussion about this post