NA MWANDISHI WETU
VIONGOZI wa Kitaifa wa Chama cha ACT-Wazalendo wakiongozwa na Kiongozi wake Dorothy Semu wanatarajiwa kushiriki kwenye Kampeni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwenye Mikoa yote ya Tanzania Bara ili kuwanadi wagombea wao.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 19,2024 mkoani Dar es Salaam,Msemaji, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa chama hicho Rahma Mwita, amesema kampeni hizo zitaanza Novemba 20 hadi 26,2024 ambapo uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
Amesema kwenye kampeni hiyo, viongozi hao wa kitaifa watawanadi wagombea wa ACT Wazalendo kwenye vijiiji na mitaa mbalimbali nchini.
Amesema Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu na Makamu Mwenyekiti Bara Isihaka Mchinjita wataongoza kampeni ya viongozi wa kitaifa kwenye mikoa ya Mkoa wa Kichama Mwambao, Lindi, Mtwara na Mkoa wa Kichama Selous.
Mwita amebainisha kuwa Kiongozi wa Chama Mstaafu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake Janeth Rithe na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Abdul Nondo wataongoza kampeni ya viongozi wa kitaifa kwenye mikoa ya Tabora, Katavi na Rukwa.
‘’Makamu Mwenyekiti Zanzibar Ismail Jussa na Mjumbe wa Kamati Kuu Rehema Ally wataongoza kampeni kwenye Mkoa wa Tanga.
‘’Katibu Mkuu Ado Shaibu na Katibu wa Ngome ya Wazee Janeth Fusi wataongoza kampeni ya kitaifa kwenye Mikoa ya Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.
‘’Naibu Katibu Mkuu Bara Ester Thomas akiambatana na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu Mbarala Maharagande wataongoza kampeni ya viongozi wa kitaifa kwenye Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Kagera na Geita’’amesema Mwita
Aidha Mwita ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama Mstaafu Juma Duni Haji ataongoza kampeni ya kitaifa kwenye mkoa wa Dar es Salaam ambapo jumla ya mikutano 28 itafanyika.
‘’Mbali na misafara hii, kutakuwa na kampeni itayoongozwa na wajumbe wa Kamati Kuu, Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mawaziri Kivuli kwenye mikoa yote ambayo imebakia.
‘’Kampeni ya viongozi wa kitaifa inakusudiwa kuongeza nguvu kwa kampeni itayofanywa na wagombea katika vijiji, mitaa na vitongoji pamoja na viongozi wetu wa matawi, kata, majimbo na mikoa’’ameongeza Mwita
Katika hatua nyingine,Mwita amefafanuwa kuwa chama chao kimeanza hatua ya kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya kufungua kesi mahakamani kupinga kuondolewa kwa wagombea wao wa vijiji, mitaa na vitongoji.
‘’Ofisi ya Katibu Mkuu imeshakiandikia Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuomba kuongezewa nguvu ya mawakili kuhakikisha tunafungua kesi dhidi ya kuenguliwa kwa wagombea wote wa vijiji, vitongoji na mitaa’’amesema Mwita



Discussion about this post