NA GOODLUCK HONGO,DODOMA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuwa chachu katika ukuaji wa Uchumi nchini kwa kujenga nyumba bora za makazi na upangaji wa miji katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yanakuja wakati ambapo NHC ikiendelea kutatua changamoto ya nyumba za makazi kupitia miradi yake mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa Nyumba 1000 za makazi katika Jiji la Dodoma.
Kazi kubwa inayofanywa na NHC inaelekea kubadilisha muonekano wa eneo na kutoa fursa kwa makumi ya wakazi ikiwemo kuboresha hadhi ya wale ambao wanaishi na watakaoishi katika makazi hayo.
Uwekezaji na Maendeleo ya Mradi wa Iyumbu Nyumba 1000 ambapo awamu ya kwanza zimeshajengwa nyumba 404 unaonekana kutoa suluhisho la makazi na kuboresha hali ya maisha kwa wakazi wake.
Kukamilika kwa mradi huo pia utasaidia kupunguza mahitaji makubwa ya nyumba na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jiji la Dodoma
Mradi huo pia utasaidia jamii kuishi katika eneo lenye miundombinu iliyoboreshwa na ongezeko la thamani ya mali ambapo mradi huo utaleta.
Hata hivyo lengo kuu la NHC ni kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora kwa watanzania .
Makazi bora na salama yamekuwa hitaji muhimu kwa maisha ya binadamu na kusababisha amani,upendo na kutimiza kwa ndoto za watu wanaotaka kuwa na makazi bora ambapo nyumba za makazi zinaweza kuwa za kupanga au kujenga huku mhusika akiwa na mamlaka juu ya makazi hayo.
Hata hivyo Watanzania wengi bado wanaishi katika nyumba za kupanga kutokana na tofauti ya kipato na changamoto wanazokutana nazo katika nyumba hizo za kupanga husababisha hali ya kuhama hama kutoka eneo moja kwenda lingine.
NHC imekuwa suluhisho kwa upatikanaji wa nyumba bora za kupanga na kununua kwa gharama nafuu,haraka na rahisi

Akizungumzia kuhusu miradi ya NHC jijini Dodoma,Meneja wa Shirika hilo mkoani humo Gibson Mwaigomole anasema Shirika lao linafanya kazi nchi nzima na karibu kazi zote katika mikoa hiyo zinafafana.
Anasema NHC inajenga nyumba na kuziuza,wanafanya ujenzi wa majengo ya makazi na biashara lakini wao pia ni wakandarasi,wanapangaji miji,washauri elekezi pamoja na kusimamia nyumba zao ambazo wamezipangisha.
Anasema usimamizi wa nyumba hizo ni katika upande wa kuzifanyia matengenezo na kukusanya kodi kutoka katika nyumba hizo ambazo ni za makazi na biashara.


‘’Katika Mkoa wetu wa Dodoma tumekuwa na miradi ambayo Shirika inaileta ya nyumba za makazi, mfano kwa hapa Dodoma tumewahi kuwa na majengo ya nyumba za makazi eneo la Medeli ambapo majengo yake tayari tumeshayauza,lakini pia tulikuwa na mradi wa Nyumba 1000 na tumefanikiwa kujenga nyumba 404.
‘’Nyumba 101 zipo Chamwino na Nyumba 303 zipo eneo la Iyumbu,Nyumba hizi za Chamwino zimekwisha uzwa zote lakini nyumba ambazo zipo Iyumbu baadhi zinaendelea kuuzwa na zingine zimekwisha uzwa.


Mwaigomole anasema bado kuna nafasi ya watanzania kuja kununua nyumba zilizobakia Iyumbu.
‘’Kwa upande wa Iyumbu,tunajiandaa kuja na Iyumbu awamu ya tatu lakini katika mradi wa Iyumbu tayari tumeshauza nyumba zaidi ya 370.
Mwaigomole anafafanuwa kuwa mbali na Iyumbu lakini pia katika eneo la Medeli watakuwa na Mradi wa Medeli awamu ya tatu,kwa kuwa katika eneo hilo walishajenga awamu ya kwanza na pili na nyumba zote zilikwisha uzwa ambapo sasa wanakuja na awamu ya tatu na ujenzi wake utaanza ndani ya miezi mitatu ijayo.


Mikakati ya NHC KUKABILIANA NA UHABA WA NYUMBA

Akizungumzia kuhusu kukabiliana na mahitaji makubwa ya nyumba,Mwaigomole anabainisha kuwa kwa sasa wameshapata ekari 48 katika eneo la Njedengwa,Nala ekari 14,Iyumbu ekari 34 ambazo bado hazijaendelezwa
‘’Hatujakaa hapa hapa tu Dodoma mjini,tumekwenda hadi wilayani,mfano eneo la Bahi tuna ekari tano,Chemba kuna ekari tano pia,lakini pia kuna Wilaya ambazo tulishafika na kujenga nyumba ambapo 42 zipo Kongwa na zote zimepangwa.
‘’Tujanaribu kwenda kila eneo na tunajaribu kupata maeneo ili tuweke uendelezaji wa nyumba na hatimaye kujaribu kukidhi mahitaji ya nyumba na tutafika kila Wilaya za Mkoa wa Dodoma”anabainisha Mwaigomole

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maeneo hayo,Mwaigomole anaongeza kuwa wao wanapata ushirikiano kutoka katika Halmashauri za Wilaya na taasisi zingine kwa kuwa wanajua NHC ipo kwa ajili ya uendelezaji wa nyumba hivyo huwapatia ushirikiano wa kutosha.
Mwaigomole amewataka watanzania na wale waishio nje ya nchi kuchangamkia fursa za nyumba za Shirika hilo kwa kuwa nyumba walizonazo zina miundombinu yote inayohitajika na gharama ni nafuu.
‘’Tunawaomba watanzania mjitokeze kwa wingi sana kujipatia nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa ,Nyumba zetu ni imara japo wengine wanasema nyumba zetu ziko bei ya juu lakini hizi nyumba mtu unainunua na kukuta miundombinu yote ipo tayari,maji yako ndani,umeme upo kila kitu kipo hivyo ni fursa ya mtu kukaa katika eneo ambalo limepangwa na zuri.
‘’Jitokezeni na hakuna sababu yoyote ya kusema uko mbali kwani Shirika letu linafanya kazi katika Mikoa 23 hivyo aliye Mkoa wa Shinyanga atafika katika Ofisi za Mkoa huo wa Shinyanga kama anahitaji nyumba Dodoma au Dar es Salaam ataonana na watumishi wetu katika eneo hilo watamsaidia.
‘’Kupitia Ofisi tulizonazo mtu anaweza kupata mahitaji anayotaka na pia tuko katika mitandao ya kijamii hivyo utapata fomu ya ununuzi wa nyumba popote ulipo na nyumba hizi ni kwa ajili ya wote’’anasema Mwaigomole

Kwa upande wake Afisa Masoko na Mauzo wa NHC Mkoa wa Dodoma Mariam Chisumo anasema katika Mradi wa Nyumba 1000 uliopo eneo la Iyumbu wamejenga nyumba za aina tatu ambapo wana nyumba za square mita 75 zikiwa na vyumba viwili ambazo zote hadi sasa zimekwisha uzwa,pia zipo za square mita 120 na 100 ambapo nyumba hizo zote zina vyumba vitatu.

‘’Katika Mradi huu wa Iyumbu tumebakiza nyumba chache hivyo tunawahimiza watanzania waje wawekeze katika huu mradi wa Iyumbu Nyumba 1000 kwa kuwa ni eneo zuri na pia wapo karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Mji wa Serikali Mtumba ambapo kwenda mjini ni karibu hivyo waje kwa wingi kuwahi fursa hiyo.
‘’Katika mradi wa Iyumba utapata huduma za kijamii ,shule za awali ambapo watoto watapata huduma nzuri bila kwenda mbali,maduka na maeneo ya kupumzika,huduma za maji ,umeme.
‘’Utapata hati kwa wakati,na huku hakuna migogoro,viwanja vyote vimepimwa na vinaanzia squere mita 500 hadi 1000”anasema Chisumo
Hata hivyo Chisumo amewatoa hofu watanzania kwa wale wanaotaka kununua nyumba za NHC kuwa wanaruhusiwa kuziendeleza kama kujenga uzio na vingine
”Kwa sasa ni Mradi wa Iyumbu pekee ndio ambao una nyumba zisizozidi 30 ambazo ziko sokoni lakini katika miradi mingine tuliyomaliza kujenga kama Medeli nyumba zake zote zimeshauzwa na watu wanaishi tayari.”anasema Chisumo
Mkazi wa Dodoma Mariam Hassan anasema nyumba zinazojengwa na NHC katika maeneo hayo zinavutia kwa muonekano na zinajengwa katika viwango vya kisasa kama zile ambazo huonekana katika nchi za ulaya.
‘’Nimeona nyumba za Medeli kwa kweli ni nzuri sana na zinavutia kwani zimepangiliwa vizuri na kuna sehemu za watoto kucheza,kupaki magari mazingira bora ya makazi kwa binadamu kuishi’’anasema Hassan
Naye Hamisi Juma anayeishi kwa ndugu yake katika eneo la Iyumbu anasema ujenzi wa nyumba hizo na mpangalio wake ni wa kisasa na unavutia kwa binadamu kuishi.
‘’Ni eneo safi na nyumba zimepangwa vizuri ni kama tuko ulaya tu na si Tanzania ukiwa katika eneo hili huwezi kuhisi kama uko Dodoma maana vitu tunavyoviona katika vymba za wenzetu huko nje ya nchi vipo hapa na kuishi sehemu kama hii pia afya.
Juma anasema hajui kama NHC inapata ruzuku kutoka kwa Serikali na inapata sawa iongezewe zaidi na kama haipati basi Serikali ilipe ruzuku zaidi ili kuendeleza ujenzi wa makazi bora kwa watanzania ambapo pia kutasaidia kuimarisha afya zao.




Discussion about this post