NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema zoezi la uteketezaji wa dawa za kulevya walizozikamata litaendelea nchi nzima, kadri mahakama zitakavyoendelea kutoa amri
Kauli hiyo imetolewa Desemba 19,2024 mkoani Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo wakati akisimamia zoezi la uteketeza wa kilogramu 614.12 za dawa za kulevya katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga, kilichopo Wazo.

Kuteketezwa kwa dawa hizo ni muendelezo wa kazi kubwa inayofanywa na DCEA katika kupambana na biashara hiyo yenye madhara makubwa kwa afya za watanzania na kiuchumi .

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uteketezaji wa dawa hizo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema , kati ya dawa zilizoteketezwa, kilogramu 601.87 ni methamphetamine na kilogramu 12.25 ni heroin ambapo dawa hizo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo.
Amesema uteketezaji huo umefanyika baada ya Mahakama za Hakimu Mkazi Kibaha mkoani Pwani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuamuru uteketezaji wake kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo wakati kesi husika bado zinaendelea.
“Uteketezaji wa dawa hizi unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni zake.
‘’Sheria hii inaruhusu uteketezaji wa dawa hizi kufanyika kabla, wakati, au baada ya shauri kumalizika mahakamani,” ameeleza Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa uteketezaji huo unafanywa kwa njia zinazozingatia usalama wa afya ya watu na utunzaji wa mazingira, huku ukisimamiwa na wadau mbalimbali waliotajwa kisheria.
Aidha, Kamishna Lyimo ameongeza kuwa katika mwezi huu wa Desemba pekee, Mamlaka imefanikiwa kuteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika Mkoa wa Tabora, pamoja na kilogramu 398.105 za dawa mbalimbali mkoani Mtwara na inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi mkoani Arusha katika siku chache zijazo.

Kamishna amewapongeza wadau wote waliofanikisha uteketezaji wa dawa hizo na kuendelea kushirikiana na mamlaka katika juhudi za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na kuwa zoezi la uteketezaji litaendelea nchi nzima, kadri mahakama zitakavyoendelea kutoa amri.
“Tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa dawa hizi haramu zinadhibitiwa kwa ustawi wa jamii yetu,” amefafanuwa Kamishna Jenerali Lyimo.




Discussion about this post