NA GOODLUCK HONGO,DODOMA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limewahimiza wapangaji wanaopanga katika nyumba za shirika hilo kulipa kodi ya pango kwa wakati ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza.
Ulipaji wa kodi hizo kwa wakati utasaidia kuendeleza miradi mingine ya nyumba za shirika hilo na kukidhi mahitaji ya watanzania wengine wanaohitaji nyumba za kupanga na kununua.
Akizungumza mwishoni mwa wiki kuhusu wapangaji jijini Dodoma,Meneja wa NHC Mkoa wa Dodoma Gibson Mwaigomole amesema ni muhimu kwa wapangaji kulipa kodi kwa wakati ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwani hilo si jambo jema kutolipa kodi hadi uchukuliwe hatua.
‘’Kama unadaiwa hakikisha kuwa unalipa deni lako la nyumba na kama una tatizo fika katika Ofisi zetu ueleze na tuzungumze na tutapeana muda ili uweze kulipa deni lako kuliko kukaa kimya hadi kufikia hali ya kutoana ndani ya nyumba.
‘’Natoa wito kwa watu kuwa na utamaduni wa kulipa kodi ili kuliwezesha Shirika kupata mapato ambayo ndiyo tunaenda kuyarudisha na kujenga hizi nyumba nyingine katika kuendelea kupunguza uhitaji wa nyumba katika nchi yetu’’amesema Mwaigomole
Kwa upande wake Afisa Miliki wa NHC Mkoa wa Dodoma Pauline Kamaghe amesema Shirika la Nyumba la Taifa linafanya shughuli nyingi sana ikiwemo kupangisha,kujenga na kuuza lakini pia kama wakandarasi na kupanga miji.

Kamaghe ambaye pia ndio Msimamizi wa Nyumba zote za NHC Mkoa wa Dodoma zikiwemo viwanja pamoja na majengo yake amebainisha kuwa kwa kitengo chao hushughulika sana na watu katika kuwapangisha nyumba zao.

Amesema kutokana na mahitaji makubwa ya nyumba,NHC kwa sasa haina nyumba iliyo wazi kwa kuwa zote zimejaa kutokana na huduma bora na gharama nafuu wanazotoa katika nyumba zao hali inayowafanya wateja wao kukaa muda mrefu bila kuhama.

‘’Mteja akifika tunamwambia jaza fomu ili uwe kwenye foleni ili mtu akitoka wewe ndio ufuate tukupangishe kwa kuwa fomu hiyo inasaidia kujua yeye ni nani,anafanya shughuli gani,anataka nyumba ya namna gani ,eneo gani na pia uwezo wake wa kulipa kodi katika nyumba tutakayompangisha.
‘’Kila mtu anaruhusiwa kupanga nyumba za Shirika na malipo ya fomu ni Sh.2500 tu na nyumba ikipatikana utakuja na kulipia malipo na utaendelea kuishi,karibuni NHC nyumba zipo lakini ni za kusubiri.Amesema Kamaghe

Akizungumzia kuhusu ulipaji wa kodi kwa wapangaji ,Kamaghe amesema wanapenda kusisitiza kuwa kila mpangaji lazima asome mkataba wake na ahakikishe kuwa ana mkataba hai.
Amesema wao kama NHC huwasikiliza wateja wao na kutatua kero zao kama wanazo na kuzifikisha kwao na mfano mzuri ni ukarabati mkubwa walioufanya katika nyumba zao zote jijini Dodoma
‘’Mkataba hai sio faida kwa Shirika bali ni kwa kila mtu,kwani unaonesha haki zote za mpangaji na Shirika lina haki zake na pia linahitaji baadhi ya vitu kutoka kwa mpangaji ambavyo vyote vimeanishwa katika mkataba.
‘’Huwa tunasisitiza sana kila mpangaji anayeingia katika nyumba awe na mkataba ambao uko hai na ni wa miaka mitatu na ukiisha unaruhusiwa kuusogeza mbele na taarifa inatakiwa kutolewa kabla ya miezi mitatu, na sisi tunasema sawa kama kutakuwa na mabadiliko ya kodi au hakuna tutakwambia katika kipindi hicho na ukikubali unaendelea.
”Kwa Dodoma tupo Jengo la Mkandarasi Ghorofa ya Sita na ukifika utapata utaratibu wote wa kupata nyumba’’anaongeza Kamaghe

Kamaghe amewakumbusha wapangaji kulipa kodi kwa wakati kwa kuwa tangu Shirika hilo limeanzishwa mwaka 1962 hadi sasa nyumba zinaendelea kuwepo na kuongezeka kwa sababu ya kodi hiyo wanayolipa ambayo inawasaidia kujenga nyumba nyingine na wengine nao waje kuishi katika nyumba za Shirika.
‘’Tulipe kodi kwa wakati,tutunze nyumba zetu na kuwa na mikataba iliyo hai,lakini pia Shirika linasikiliza ushauri na kuufanyia kazi kutoka kwa wapangaji wetu na mfano walishauri ukarabati na tumefanya hivyo na wanaishi sehemu nzuri na safi.
‘’Kodi yetu sisi tunachukua kila mwezi na ikitokea mpangaji hajalipa huwa tunampatia taarifa ya siku 30,ikifika tena mwezi wa pili ambapo itakuwa imetimia siku 60 na hujalipa tunakupeleka kwa Dalali wa Mahakama na yeye atatoa siku 14 ili mpangaji alipe’’ameeleza Kamaghe

Kamaghe amebainisha kuwa ikiwa miezi yoyete mitatu hajalipa na siku alizopewa na Dalali wa Mahakama hajakamilisha basi wao NHC wataita Serikali ya Mtaa na kumuondoa katika nyumba.





Discussion about this post