NA GOODLUCK HONGO
MKOA ya Mara umetajwa kuongoza katika kilimo cha dawa za kulevya aina ya bangi ikifuatiwa na Morogoro huku Katavi ikishika nafasi ya mwisho kati ya 11 iliyoorodheshwa.
Mwaka 2024 kiasi cha bangi tani 2,303.20 ilikamatwa ambapo mirungi ilifikia tani 18.45
Hata hivyo Mkoa wa Mtwara umeshika nafasi ya tatu kwa kulima dawa hizo za kulevya huku Mkoa wa Iringa ukishika nafasi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 iliyotolewa Juni,2025 na kuwekwa saini na Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge na Uratibu) William Lukuvi pamoja na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)Aretas Lyimo imeeleza ekari za mashamba ya bangi zilizoharibiwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa mwaka 2024.
Katika taarifa hiyo imeonesha kuwa jumla ya ekari 3,045 ziliharibiwa katika Mkoa wa Mara pekee ambapo Mkoa wa Morogoro ukiwa na ekari 1,165 zilizoharibiwa kwa mwaka 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Mkoa wa Mtwara ziliharibiwa jumla ya ekari 157 ikifuatiwa na Mkoa wa Arusha ukiwa na ekari 131 ambapo Mkoa wa Tabora ziliharibiwa ekari 103.
Mikoa mingine ambapo mashamba ya bangi yaliharibiwa ni pamoja na Shinyanga ekari 67,Lindi ekari 35,Dodoma ekari 14,Ruvuma ekari saba,Iringa nne na Katavi ekari tatu.
Hata hivyo bangi imeonekana kuongoza katika kesi zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini ambapo mwaka 2024 pekee jumla ya kesi 850 zilifunguliwa zikifuatiwa na dawa za kulevya aina ya mirungi ikiwa na kesi 340 huku watuhumiwa 7,981 wakikamatwa wakiwemo wa mirungi 1,256
Katika taarifa hiyo mikoa ya Mwanza,Pwani,Kagera,Rukwa,Mbeya,Geita,Dar es salaam,Singida,Manyara,Tanga na Kilimanjaro haikutajwa.
Hata hivyo kukamatwa kwa idadi kubwa ya watuhumiwa kunaonesha ni jinsi gani kazi kubwa inafanyika kutokomeza uhalifu huo ambapo watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za kisasa na kisayansi katika kufanikisha biashara hiyo.




Discussion about this post