NA MWANDISHI WETU
ATHARI za kutanuka kwa Mto Msimbazi zimeendelea kuathiri maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kutokana na makumi ya nyumba kusombwa yakiwemo makaburi.
Hali hiyo inatokana na mmomonyoko wa ardhi katika baadhi ya maeneo ambapo sasa unatishia uhai wa mji wa Vingunguti huku hali hiyo ikiathiri makazi ya watu na barabara ya kiwango cha lami katika eneo hilo baada ya kingo zake kuendelea kutanuka.
Uchunguzi uliofanywa na Bajeti Communication umegundua kuwa athari za Mto Msimbazi katika maeneo ya Kipawa,Ulongoni,Tabata pamoja na Vingunguti ni mkubwa baada ya makumi ya nyumba kuanguka na kusombwa na maji huku nyingine zikiwa hatarini kuanguka.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia hali hiyo,wamesema kuwa katika eneo la Butiama pekee nyumba zaidi ya 60 tayari zimeshaondoka na kupotea kutokana na kutanuka kwa mto huo.

Akizungumzia hali hiyo,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Butiama uliopo katika Kata ya Vingunguti jijini Dar es Salaam Elvis Bwahama amesema atahari za mto huo ni kubwa lakini wanaishukuru Serikali kwa kumpeleka mkandarasi ambaye atasafisha mto huo na kujengea kingo zake kwa pande zote za mto huo.

Amesema mbali na nyumba kubomoka lakini pia makaburi nayo yamekumbwa na athari hiyo hali iliyoifanya Serikali kuyahamishia katika maeneo mengine.
“Makaburi nayo mengi yaliondoka lakini Serikali ilikuja na mkakati wa kuyahamisha makaburi na mengine yamebakia na mengine yamepelekwa maeneo ya Kinyerezi,lakini ni ukweli nyumba nyingi ziliondoka”
“Sababu kubwa ya huu mto kutanuka ni uchimbaji wa mchanga lakini pia mto huu haujanyooka,yaani unahama (Zigzag) katika pia hata wananchi waliojenga makazi yao bondeni pia wanasababisha huu mto kuleta uharibifu”amesema Bwahama

Bwahama ameongeza kuwa awali walijaribu kuweka taka katika kingo za mto huo lakini hazikusaidia chochote na sasa wamezuia na pindi wanapowakamata wananchi wanaomwaga taka hizo wanakamatwa na wengine wanalipishwa faini pamoja na kufikishwa mahakamani.
“Kwa sasa kuna nyumba kama saba ambazo zimefanyiwa tathmini ili kuhamisha barabara hiyo iliyomeguka lakini pia kuna mradi wa uboreshaji wa Mto Msimbazi kutoka Benki ya Dunia nayo tunasubiri lakini pia kuna mkandarasi ambaye tayari ameshapatikana.
“Awali mkandarasi alijenga gati na zilisaidia zaidi na sasa atajenga gati mitaa yote ambayo imepitiwa na Mto Msimbazi.
“Pamoja na juhudi ambazo Serikali imezifanya bado tunaendelea kuiomba kwa jicho la huruma waendelee kutusaidia kutekeleza hili jambo kwani wananchi wanaathirika nyumba zao zinaondika hivyo tunaomba watupe kipaumbele kutusaidia kwa kuuboresha huu mto”amebainisha Bwahama





Discussion about this post