NA MWANDISHI WETU
RAIA nane kutoka nchini Pakistan wamekamatwa nchini kwa kujihusisha na dawa za kulevya wakiwemo pia kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo(DRC) na Visiwa vya Comoro.
Raia wengine waliokamatwa ni pamoja na raia kutoka Brazil ambapo kwa pamoja wanajumuisha watuhumiwa ambao ni raia wa kigeni kufikia 11.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 iliyotolewa Juni,2025 na kuwekwa saini na Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge na Uratibu) William Lukuvi pamoja na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuwa raia wa kigeni 11 walikamatwa nchini kwa kujihusisha na dawa za kulevya.
“Mwaka 2024,raia wa kigeni 11 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya,kati yao nane walitoka katika Nchi ya Pakistan ,mmoja kutoka visiwa vya Commoro,mmoja kutoka Nchi ya Congo na mwingine kutoka Nchi ya Brazil wote wakiwa wanaume”imeeleza taarifa hiyo
Kwa upande wa watanzania waliokamatwa nje ya nchi kwa kujihusisha na dawa za kulevya,taarifa hiyo imefafanuwa kuwa takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa jumla ya watanzania watano walikamatwa.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa wawili kati yao walikamatwa nchini Afrika Kusini,wawili nchini India na mmoja nchini Burundi wote wakiwa ni wanaume.
Hata hivyo idadi ya watanzania imeendelea kushuka katika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambapo kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa Mwaka 2023 imeonesha kuwa ni watanzania 26 pekee ndio waliokamatwa nje ya nchi kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.




Discussion about this post