NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha African Democratic Alliance(ADA-TADEA) kimeeleza kuwa kitawalipa askari wote walioshiriki vita vya Kagera kiasi cha Sh.Milioni saba kila mmoja endapo kitachaguliwa na wananchi kushika dola katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025.
Mbali na hilo lakini pia kitaunda chombo madhubuti kinachojitegemea na chenye uwezo wa kufanya kazi za kijasusi duniani ikiwemo pia Taasisi ya Upelelezi Tanzania (TUTA).
Hayo yamebainika ndani ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025-2030 ya chama hicho iliyozinduliwa Septemba 14,2025 Mbagala mkoani Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuzindua kampeni za urais,ubunge na udiwani ili kuwanadai wagombea wao nchi nzima.
Ilani hiyo yenye kauli mbiu “Uhuru na Uwajibikaji, Tanzania Mpya yenye Utajiri wa Haki na Amani”imeeleza kuwa katika suala la mabadiliko ya ulinzi na usalama wao hawana Mjomba wala Shangazi wa kuwaonea huruma au kuwabeba bali ni wao wenyewe kujisimamia.
Ilani hiyo imebainisha kuwa ili kuwa salama inabidi kuangalia masuala matatu ambayo ni Usalama wa Taifa ,Jeshi la Wananchi na Usalama wa Raia.
“Kitu cha msingi ambacho tutakifanya ni kuwalipa askari wote walioshiriki vita vya Kagera ,sasa ni zaidi ya miaka 40 askari hao hawajalipwa.
“Cha kushangaza fedha zilitolewa ,inadaiwa kuwa walilipwa lakini wanajeshi wenyewe wanalalamika hadi leo,kwa sababu hakuna ushahidi kama walilipwa au hakuna nyaraka zinazoonesha waliweka saini kupokea malipo hayo ,tuna imani hawajalipwa .
“Hivyo sisi tutawalipa wote kutokana na ukweli kuwa orodha yao ambayo ipo,na watalipwa Shs.Milioni saba(7,000,000/=) kila mmoja badala ya Shs.Elfu tano(5,000/=) walizodaiwa kulipwa ,kwani walifanya kazi kubwa ya kizalendo kulipa ushindi Taifa letu”imebainisha Ilani hiyo
Aidha imeogeza kuwa itaunda chombo madhubuti kinachojitegemea na chenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi za kijasusi duniani ambacho ni Wakala wa Tanzania wa Ujasusi (WATU) Tanzania Agency for Intelligent (TAI)

Hata hivyo chama hicho kupitia Ilani yake imejipanga kuhakikisha kuwa itabadilisha mtazamo wa Jeshi la Polisi na Magereza kuwa ni kujali utu na maslahi ya wananchi zaidi ikiwemo kuunda Taasisi ya Upepelezi Tanzania(TUTA)-Bureau of Investigation ina Tanzania (BIT)
“Taasisi hiyo itajitegemea tofauti na Polisi ila itashirikiana na vyombo vingine vya usalama,Polisi italazimika kuwa makini na rafiki wa raia ili iweze kufanya kazi zake vizuri.
“Iwe ni marufuku kwa Polisi kufanya unyanyasi kwa raia na wanapaswa kuzingatia usalama wa Raia na Mali zao kwa kuheshimu utu na heshima za watu na haki za binadamu kwa mujibu wa sheria”imefafanuwa Ilani hiyo
Mwenyekiti wa ADA-TADEA na mgombea wa urais Zanzibar Juma Ali Khatibu amesema kuwa Ilani ya chama chao imejiwekea mtanzamo maalum kwa upande wa Zanzibar
Amebainisha kuwa lengo kubwa ni kuendelea kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ,kuimarisha Muungano ili kujenga msingi imara wa kiuchumi na siasa kwa kuthamini utamaduni,mila na desturi ili kuwa na Tanzania Mpya yenye utajiri,haki na amani.
“Nia yetu kuu ni kuwaunganisha wananchi ili washirikiane kukuza uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla.
“Kwa heshima ninawaomba kura zenu za NDIYO kwangu kama Mgombea wa kiti cha Urais Zanzibar,Ndugu Georges Gabriel Bussungu ,Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania na uwezo katika nafasi za Ubunge,Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani.
“ADA-TADEA itatumia fursa muhimu kwa Zanzibar kuwa na Utalii wa mikutano na kinachotakiwa baada ya sisi kuchaguliwa ni kuweka miundombinu mizuri katika maeneo ya kufanyia mikutano hiyo”amesema Khatibu
Katibu Mkuu wa Chama hicho Salehe Msumari ameelezea ilani yao kuwa ni bora kuliko za vyama vingine na kwamba ADA-TADEA kimekuwa na kuendeela kupanuka kutokana na hamu ya wananchi kujikomboa kutoka kwenye uchumi hodhi,utumwa wa fikra za ukoloni mambo leo na nguvu ya ubeberu
“Chama hiki kiliundwa kwa lengo la kuleta mabadiliko kawa amani ya kisiasa nchini Tanzania yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Tanzania African National Union (TANU) na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa awamu ya kwanza Hayati Oscar Salathiel Kambona(1925-1997)”amesema Msumari




Discussion about this post