NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA) kimesema katika siku 100 za kwanza kuingia madarakani kitaweka utaratibu wa mfumo wa Serikali tatu katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbali na hilo lakini pia CHAUMMA itawasilisha bungeni Mswada wa Marekebisho ya Sheria kwa ajili ya kuondoa utaratibu uliowekwa na sheria w Kikokotoo na kurudisha wa zamani.
CHAUMMA imebainisha hayo kupitia Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu 2025-2030 iliyotiwa saini na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalim Salum Juma ikielezea mfumo wa utalawa ambapo kitajikita katika kuheshimu mgawanyo wa mihimili ya dola kwa mujibu wa Ibara ya 4(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwa kuhakikisha kwamba mihimili ya dola yaani Serikali,Bunge na Mahakama inatekeleza majukumu yake bila kuingilia.
Hata hivyo CHAUMMA imebainisha kupitia Ilani yake kuwa inaamini katika mfumo wa Serikali tatu yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
“Katika siku 100 za kwanza za utawala ,CHAUMMA itahakikisha kwamba inaweka utaratibu wa kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo utaratibu wa mfumo wa Serikali tatu utawekwa rasmi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “imebainisha Ilani hiyo.
Kwa upande wa watumishi wa umma,Serikali ya CHAUMMA itahakikisha kuwa katika siku 100 za kwanza madarakani inawasilisha Bungeni muswada wa marekebisho ya sheria kwa ajili ya kuondoa utaratibu uliowekwa na sheria wa Kikokotoo
“Tutarejesha utaratibu na fomula ya zamani ili kuwawezesha watumishi wa umma wanapostaafu kuweza kuanza maisha mapya badala ya mfumo wa sasa unaowalazimisha watumishi kulipwa kidogo kidogo mafao yao jambo ambalo linapelekea wastaafu wengi kushindwa kupanga maisha mapya baada ya kustaafu utumishi wa umma”imeeleza Ilani hiyo
Ilani hiyo pia imeongeza kuwa kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kupandishwa madaraja ,Serikali ya CHAUMMA itahakikisha kuwa inawapandisha madaraja kwa wakati na kuwalipa stahiki zao katika muda muafaka ili kuwaondolewa manung’uniko wakiwa kazini.
“Ilani hii ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025-2030 imejengwa kwa dhati ya kutatua na kumaliza kero zote zinazoukabili umma wa watanzania.
“Ni dira ya maendeleo makubwa yenye lengo la kushika dola ili kufanikisha malengo ya chama chetu kujenga Tanzania yenye uongozi wa maadili,uchumi shirikishi na jumuishi,jamii yenye haki sawa ,na Taifa lenye maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo”imefafanuwa Ilani hiyo.
Watanzania wanatarajiwa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025 na kumchagua Rais,Wabunge na Madiwani wataohudumu kwa muda wa miaka mitano hadi 2030 ambapo vyama 18 vinashiriki.



Discussion about this post