CAIRO,MISRI
MZOZO wa ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme wa maji lililojengwa na Ethiopia katika Mkondo wa Mto Nile umeendelea kuchukua sura mpya baada ya Misri kusisitiza kuwa limejengwa kinyume cha sheria.
Mzozo wa bwawa hilo kati ya Ethiopia na Misri ikiwepo na Sudan ulianza mwaka 2011 baada ya Ethiopia kutangaza ujenzi wa bwawa wake walilolipa jina la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) linalojulikana pia kama Al-Nahda,lenye likiwa na thamani ya dola bilioni tano za kimarekani.
GERD lililojengwa takriban kilomita 45 (maili 28) mashariki mwa mpaka na Sudan kwenye Blue Nile ambao ni mkondo mkuu wa Mto Nile.
Bwawa hilo limekuwa likijengwa tangu mwaka 2011 ili kuzalisha takriban megawati 6,000 za umeme kwa mwaka ikiwa na mitambo 13 likiwa na urefu wa mita 145 na upana wa mita 1,800, huku likiwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo bilioni 70 za maji kwenye hifadhi yake
Hata hivyo Misri imekuwa ikishikilia umiliki wa maji ya Mto Nile na kuwa hakuna nchi zingine zenye mamlaka ya kutumia maji ya mto bila makubaliano na Misri.
Kitendo cha Misri kulazimisha matumizi ya maji ya mto huo bila idhini yake kumechochea mgogoro zaidi.
Misri mara kadhaa imetishia kuchukua hatua dhidi ya nchi zinazoonekana kutumia maji ya mto huo bila idhini yake.
Hata hivyo mwaka 2021 Jeshi la Ethiopia lilionya kuwa lipo tayari kulinda bwawa hilo ikiwa kutakuwa na hujuma.
Onyo hilo lilitolewa na Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Ethiopia, Meja Jenerali Yalma Merdasa, ambaye aliongeza kwamba kikosi hicho hakijatoa jicho lake kwenye Bwawa la Renaissance hata kwa dakika moja, na kwamba kiko tayari kulinda usalama wa anga wa nchi hiyo.
Meja Jenerali Merdasa aliongeza kuwa, “Kikosi cha Anga na Kikosi cha Ulinzi cha Ethiopia kwa masaa 24, kimeelekeza macho yake angani na hakijatoa macho yake kwenye Bwawa la Renaissance.
Amesisitiza kuwa, kikosi hicho kiko tayari kuzuia shambulio lolote linalotaka kuharibu nchi, kulingana na maagizo yaliyotolewa na ngazi za juu.
Mbali na onyo hilo la kijeshi lakini pia mwaka 2021 Ethiopia ilituma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikilalamika kuwa Misri na Sudan hazina nia njema katika mazungumzo yanayohusu Bwawa la Grand Rainissance la Ethiopia (GERD) ambalo pia linajulikana kama al-Nahdha
Misri inasisitiza kuwa Bwawa la GERD la Ethiopia limejengwa “kinyume cha sheria” na inahifadhi haki yake ya kuchukua hatua zozote inazoziona kuwa muhimu kulinda usalama wake wa maji.
Wakati Misri na Sudan zipinga ujenzi wa bwawa hilo ambalo Ethiopia inaeleza kama chanzo chake cha kulipatia taifa hilo maendeleo kupitia nishati,Misri tayari inamiliki bwawa la Aswan High ambalo nalo limejengwa katika mto Nile.

Hivi karibuni Waziri wa Umwagiliaji na Rasilimali za Maji wa Misri, Hani Sewilam amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari kuwa kukamilika kwa bwawa hilo na kupita kwa muda hakumaanishi kuwa Misri imekubali hali hiyo au kuachana na haki zake
Sewilam hayo wakati wa mkutano jijini Cairo na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kigeni nchini Misri.
Amesema Azimio la Kanuni za 2015 lililotiwa saini na Misri, Ethiopia, na Sudan lilikusudiwa kuwa mwongozo wa kuweka ahadi za ushirikiano, kufikia makubaliano kuhusu ujazaji wa awali wa bwawa hilo na uendeshaji wa kila mwaka, pamoja na uratibu na kubadilishana taarifa.
Sewilam amesema azimio hilo haliipi Ethiopia haki ya kuchukua hatua za upande mmoja kuhusu bwawa hilo, na kuongeza kuwa Misri inachukulia mwendelezo wa ujazaji na uendeshaji bila makubaliano kama ukiukaji wa ahadi hizo.
“Bwawa hili ni kinyume cha sheria, Misri ina haki ya kuchukua hatua mwafaka ili kuondoa madhara yanayosababishwa kwake.”amesema Sewilam
Sewilam ameonya kuwa uendeshaji wa bwawa hilo bila uratibu unaweza kusababisha ongezeko la ghafla au kupungua kwa kasi kwa mtiririko wa maji, jambo linaloweza kuathiri mabwawa katika nchi za Misri na Sudan.
Pia amekanusha madai ya Ethiopia kwamba Misri inapokea “sehemu kubwa zaidi” ya maji ya Mto Nile.
Amesema mgao wa kila mwaka wa Misri wa bilioni 55.5 za mita za ujazo unawakilisha takriban asilimia 2.7 ya karibu trilioni mbili za mita za ujazo za mvua zinazonyesha katika Bonde la Mto Nile.
Sewilam amebainisha kuwa Ethiopia ina zaidi ya hekta milioni 18 za ardhi ya kilimo ikilinganishwa na takriban hekta milioni 4.03 za Misri.
Misri na Sudan zimetoa wito wa kuwepo kwa makubaliano ya kisheria ya pande tatu kati ya Misri, Sudan, na Ethiopia kuhusu ujazaji na uendeshaji wa bwawa hilo ili kuhakikisha haki zao za maji na maslahi yao hayadhuriki.
Hata hivyo, Ethiopia inasema kuwa uendeshaji wa bwawa hilo hauhitaji makubaliano na Sudan au Misri


Discussion about this post