LA PAZ,BOLIVIA
RAIS wa zamani wa mpito wa Bolivia Jeanine Anez amefanya jaribio la kujiua akiwa mahabusu siku moja baada ya kufunguliwa mashtaka ya “mauaji ya halaiki”
Rais huyo wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi hiyo, amefunguliwa mashitaka kutokana na vifo vya waandamanaji vilivyotokea mwaka 2019.
Wakili wa Anez, Jorge Valda, amesema kiongozi huyo wa zamani ambaye amefadhaishwa na tuhuma zinazomkabili alijaribu kujiua lakini jaribio hilo lilishindwa.
Anez, amekuwa gerezani tangu mwezi Machi mwaka huu kwa madai ya kufanya mapinduzi dhidi ya mtangulizi wake na rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales.
Anez aliingia madarakani kama kiongozi wa mpito mwaka 2019 baada ya Morales kujiuzulu na kuikimbia nchi hiyo lakini wapinzani wanasema hatua yake ya kuchukua madaraka ilikuwa sawa na mapinduzi.
Hata hivyo Disemba 31,2019, serikali yake iliamua kuwafukuza mabalozi wa ngazi za juu wa Mexico na Uhispania, baada ya jaribio la maafisa wa serikali ya zamani kuondoka kwenye ubalozi wa Mexico kwa msaada ya balozi wa Uhispania na kutoroka nchi.
Rais huyo mstaafu alisema kuwa Balozi Maria Teresa Mercado wa Uhispania na afisa wa ubalozi huyo anayehusika na usalama hawatakiwi kuwapo Bolivia ndani ya masaa 72 yajayo.
Uhispania nayo iliwafukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Bolivia kujibu hatua hiyo.
Maafisa tisa wa serikali ya Rais Evo Morales iliyopinduliwa kufuatia maandamano ya umma na uingiliaji kati kijeshi, ambao waliomba hifadhi kwenye ubalozi wa Mexico.
Serikali ya mpito ya Bolivia iliwafungulia mashitaka maafisa hao wakiwatuhumu kwa uchochezi, ugaidi na wizi wa kura, na imewakatalia kutoka nje ya nchi.
Januari 25,2020 ,serikali ya Rais Anez, ilivunja mahusiano ya kidiplomasia na Cuba na kuwarudisha nyumbani watoa huduma za afya kutoka Cuba zaidi ya 700 waliokuwa nchini humo.
Machi 13,2021 Anez,alizuiliwa kwa mashtaka ya ugaidi,ghasia na njama ndani ya upeo wa uchunguzi unaojulikana kama “kesi ya mapinduzi”.
Kulingana na habari ya gazeti la Elpais, serikali ya Bolivia ilitangaza kuwa Anez, ambaye hati ya kukamatwa kwake ilitolewa, alikuwa akizuiliwa katika eneo la Trinidad mkoani Beni.
Kama sehemu ya uchunguzi, hati ya kukamatwa ilitolewa kwa Anez, Waziri wa zamani wa Serikali Arturo Murillo, Waziri wa zamani wa Utawala Yerko Nunez, Waziri wa zamani wa Sheria Alvaro Coimbra, Waziri wa zamani wa Ulinzi wa zamani Luis Fernando Lopez na Waziri wa zamani wa Nishati Rodrigo Guzman.
Ilitangazwa kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa sababu ya uwezekano wa maafisa wa serikali wa zamani wanaotuhumiwa kwa ugaidi, uasi na njama ya kutoroka nchini na kuzuia mchakato wa uchunguzi.
Kufuatia hati ya kukamatwa, Coimbra na Guzman walizuiliwa katika mkoa wa Beni nchini humo kama sehemu ya uchunguzi, ambao Rais wa zamani Evo Morales aliuelezea kama “mapinduzi” na akachunguza sababu zilizopelekea kujiuzulu kwake, na kusema kuwa mawaziri hao wawili wangehamishiwa mji Mkuu wa La Paz.
Kwa upande mwingine, Anez, alichapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya hati ya kukamatwa, na kudai kwamba chama tawala kiliamua kurudi kwenye udikteta, kwa kutumia “mateso ya kisiasa na dhuluma.
Novemba 13,2020 Anez ambaye alikuwa makamu wa pili wa Rais wa Bunge la Seneti alijitangaza kuwa rais wa mpito wa Bolivia, licha ya kukosekana kwa idadi ya wabunge inayohitajika, akisema ameamua hivvo kutokana na kwamba kuna ” umuhimu wa kuweka mazingira sawa ya amani ya kijamii”.
Muda mfupi baada ya Anez kujingaza rais wa mpito,Morales alijibu kwa kusema kuwa jaribio la mapinduzi la kushangaza na la aibu katika historia ya Bolivia limefanyika.

Amesema Seneta kutoka mrengo wa kulia uliofanya jaribio la mapinduzi amejitangaza kuwa rais wa Seneti, kisha kaimu rais wa Bolivia bila idadi inayohitajika ya wabunge kupasisha tangazo lake, huku akizungukwa na kundi lililohusika katika jaribio hilo la mapinduzi na kuongozwa na jeshi na polisi wanaokandamiza raia.
Discussion about this post