MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kutatua migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ukiwemo wa Msitu wa Pugu Kazimzumbwi na wananchi.
Amesema ni lazima migogoro kama hiyo ifike mwisho kwa kuwa kudumu kwa muda mrefu kwa migogoro hiyo kunarudisha nyuma maendeleo.
Makalla ameyasema hayo jijini Ilala Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa ziara ya kusikiliza kero na kutatua migogoro ya wananchi ambapo leo ni zamu ya Jimbo la Ukonga
Amesema ni muhimu mgogoro wa Msitu wa Pugu Kazimzumbwi ufike mwisho na kuwataka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kupunguza matumizi makubwa ya nguvu.
“Azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kushughulikia migogoro ya wananchi, sasa tutakutana na Wizara tatu za Ofisi ya Rais Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi ili kupata ufumbuzi”amesema Makalla.
Makalla amefafanua kuwa wakati anaendelea kushughulikia mgogoro huo ni vyema TFS ikashirikiana na Wananchi hao na kuongeza kuwa ni marufuku vitendo vya kukamata Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam kuwapeleka Wilaya ya Kisarawe mkoani wa Pwani.
Miongoni mwa vilio vya wananchi hao ni matukio ya kupigwa, kuteswa na kukamatwa kwa Wakazi wanaozungukwa na Msitu huo.

Hata hivyo TFS imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa Misitu inalindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria hali inayofanya kuendelea kuonekana hadi sasa na baadhi ya misitu kutumika kama sehemu ya utalii na kuhifadhi wanyama,wadudu na uoto wa asili.
Licha ya juhudi hizo lakini pia baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa mazao ya Misitu wamekuwa chanzo cha TFS kutumia nguvu kuwadhibiti kutokana na kuharibu misitu kwa kujiangalia wao binafsi na si ya Taifa na vizazi vijavyo.
Discussion about this post