MBUNGE wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro Joseph Tadayo ameiomba serikali kusaidia changamoto ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe kutokana na eneo kubwa kumezwa na majani hayo.
Ziwa hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,lipo hatarini kutoweka kutokana na eneo kubwa la ziwa hilo kumezwa na magugu maji.
Ombi la Mbunge huyo limetolewa leo wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande ya kukagua hali ya ziwa hilo.
Tadayo amesema licha ya wao kufanya juhudi za kupambana na magugu hayo lakini ni muhimu pia kwa serikali ikaongeza nguzu zaidi kutokana na ziwa hilo kutegemewa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo Uvuvi wa Samaki,Mradi mkubwa wa Maji katika Wilaya ya Same, Mwanga,Korogwe pamoja na miradi mikubwa ya Kilimo cha Umwagiliaji.
“Ziwa hilo lina umuhimu sana kutokana na miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme,miradi ya maji na kilimo zinategemea ziwa hili na endapo hatua za haraka hazitachukuliwa miradi yote inayotegemea maji kutoka ziwa hilo zitakufa,”amesema Tadayo
Amefafanua kuwa kikubwa kinachotakiwa ni kuondoa yale magugu maji ili wananchi waendelee na shughuli zao za Uvuvi na Halmashauri kuendelea kupata mapato yanayotokana na uvuvi.
Amebainisha kuwa Ziwa hilo litasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kunufaisha wakazi zaidi ya 2564 wanaolizunguka pamoja na baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Moshi vijijini.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande amesema kutoweka kwa ziwa jipe kunaweza kukawa na madhara makubwa kwa Taifa na kupoteza fursa za uwekezaji kwa wananchi.
Hata hivyo Chande alimtaka Tadayo kushirikiana kwa pamoja ili waweze kuondoa magugu hayo ndani ya ziwa hilo ili liendelee kutoa huduma kwa wananchi wa jimbo hilo na Wilaya zingine kwa vizazi vya sasa na vijavyo


Discussion about this post