NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Serikali imetenga Sh.Bilioni 23.36 ya Wizara ya afya kwa mwaka 2022/23 na kutenga vyumba 100 vitakavyosaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) ili kupunguza vifo vyao.
Dkt.Mpango ameyasema hayo jana Julai 25,2022 jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojihusisha na kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) Doris Mollel.
Amesema serikali imeendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya katika kata pamoja na zahanati katika vijiji ili kuendelea kukabiliana na changamoto za vifo vya mama na mtoto.
Dkt.Mpango ametoa wito kwa wadau, taasisi za dini pamoja na wananchi kwa ujumla kulipa kipaumbele suala la kuwasaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ili kukabiliana na changamoto ya vifo vinavyotokana na hali hiyo.
Aidha Dkt.Mpango ameongeza kuwa ni muhimu pia kwa taasisi inapaswa kuwekeza pia katika utoaji elimu ya afya ya uzazi ili kukabiliana na ongezeko la Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwani maeneo mengi hasa ya vijijini wanashindwa kupata uelewa juu jambo hilo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojihusisha na kusaidia Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) Doris William Mollel jijini Dar es Salaam jana (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation Doris Mollel amempongeza Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango kwa jitihada alizofanya za kutambua changamoto zinazojitokeza katika malezi ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kuchangia vifaa tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hivi karibuni.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo husasani katika ajenda ya mtoto njiti na tayari wamewasilisha ombi la kuongezwa likizo kwa wanaojifungua kabla ya wakati ikiwemo kuwekwa elimu ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika masomo ya sayansi kwa shule za msingi na baiolojia kwa shule za sekondari.




Discussion about this post