NA MWANDISHI WETU
JUKWAA la Tume za Uchaguzi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (ECF – SADC) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameandaa mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo Makamishna wapya na maafisa waandamizi wa Tume ambazo ni wanachama wake.
Mafunzo hayo yaliyoanza leo Novemba 22,2022 jijini Dar es Salaam yanatarajiwa kumalizika Novemba 25, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele amesema nchi tisa wanachama wa Jukwaa la ECF-SADC ambao ni Zambia, Eswatini, Ushelisheli, Botwana, Namibia, Zimbabwe, Lesotho, Malawi na Tanzania wanashiriki mafunzo hayo.
Aidha Jaji Mwambegele amesema baadhi ya nchi ikiwemo Afrika Kusini zitashiriki katika mafunzo hayo kwa njia ya mtandao (Virtually).
Amesema wajumbe na maafisa waandamizi wa Tume za Uchaguzi watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia katika kuboresha utekelezaji wa majukumu yao.
“Washiriki watajifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ambayo uchaguzi umekuwa ukifanyika katika nchi zao na kuona changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza na namna ya kuzitatua,”amesema Jaji Mwambegele.
Aidha Jaji Mwambegele ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa amezitaja mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo kuwa ni pamoja na demokrasia, uchaguzi na menejimenti ya uchaguzi, vigezo vya kimataifa vya upimaji wa uchaguzi na wajibu wa kuendesha chaguzi za kidemokrasia; Usimamizi wa uchaguzi: Tafsiri, mifano, majukumu na na nguvu ya kisheria.
“Mada nyingine ni pamoja na Mifumo ya Uchaguzi, Mzunguko wa Uchaguzi, Kalenda ya Uchaguzi na Mipango ya Uchaguzi, Matumizi ya TEHAMA katika chaguzi, Masuala yanayojitokeza katika usuluhishi wa migogoro ya uchaguzi na utoaji haki za katika uchaguzi na Uandikishaji wa wapiga kura.
“Pia zipo mada za Siku ya Uchaguzi (Kupiga kura) na Menejimenti ya Matokeo, Changamoto kwa Tume za Uchaguzi, Uongozi wa Tume za Uchaguzi, Utendaji kazi na Uendelevu wake, Ushawishi kwa Wadau wa Uchaguzi, Changamoto na Uhusiano na Tume, Kuendesha Uchaguzi Jumuishi kwa kuzingatia Jinsia, Vijana na Watu wenye Ulemavu”amefafanua Jaji Mwambegele
Jaji Mwambegele amezitaja mada zingine kuwa ni pamona na Menejimenti ya Mashinikizo ya Kisiasa, Kugharamia Uchaguzi na Tume za uchaguzi,Ushirikiano kati ya Tume za Uchaguzi na Vyombo vya Habari na Mawasiliano ya nje ya Taasisi pamoja na masuala yanayojitokeza katika sekta ya mawasiliano ya kidigitali.
Aidha ameongeza kuwa mada zingine ni zile za kukabiliana na majanga na kujenga uwezo wa namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza na usalama wakati wa uchaguzi, vurugu na namna ya kutatua changamoto pia zitatolewa.
“Baada ya kupatiwa mafunzo ni matarajio kuwa watendaji hawa watakwenda kuhakikisha kuwa chaguzi zinakuwa huru, za haki na zenye kuaminika na hii itasaidia katika kukuza demokrasia itakayochochea amani, usalama na ustawi wa wananchi na Taifa”amebainisha Jaji Mwambegele.




Discussion about this post