NA MWANDISHI WETU,DODOMA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ametoa wiki mbili kwa mkandarasi Kampuni ya SUMA JKT kuhakikisha wanakamilisha kazi katika jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais.
Jafo ametoa kauli hiyo Februari Mosi,2023 jijini Dodoma baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais unaoendelea katika eneo la Mtumba .
Jafo ambaye aliambatana na viongozi na wataalamu kutoka Ofisi hiyo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo hilo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi.
Kwa mujibu wa mpango kazi uliowekwa, kazi ya ujenzi huo kwa ujumla iko nyuma kwa siku 41 hali inayotokana na kasi ya ujenzi wa jengo hilo kutokuwa ya kuridhisha.
Kutokana na hali hiyo Dkt. Jafo ametoa wiki mbili kwa mkandarasi Kampuni ya SUMA JKT pamoja Msimamizi Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kusiliba (plasta) kuta ambayo ilipaswa kuwa imekamilika.
Amesema kuwa pamoja na kuwa wameaminiwa na kupewa dhamana ya ujenzi wa jengo hilo la Serikali lakini haijaonesha umakini katika utekelezaji wa mradi huo.
“Hapa mko nyuma sana wenzenu kule wako mbali sana kuliko ninyi na mara ya mwisho tulipokutana mkaniambia kazi itaenda kwa kasi lakini ndio mkaamua kabisa kusimama na mmeanza tena kufanya baada ya kusikia ninakuja kukagua, hapa naona hakuna userious katika kufanya hii kazi,” ameeleza Dkt. Jafo.
Aidha amebainisha kuwa Serikali haitavumilia kuona kazi hiyo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais inakwama na kuonya kuwa kama hawataonesha maendeleo mkataba utavunjwa ili apewe mkandarasi mwingine atakayefanya kazi hiyo.
Katika ziara hiyo, Waziri Jafo pia alitembelea majengo mengine yanayojengwa na SUMA JKT na kubaini ujenzi wake unakwenda kwa kasi hivyo akaonya kuchukua hatua ya kuvunja mkataba.
Ofisi ya Makamu wa Rais ilisaini mkataba wa Sh. Bilioni 18.8 na Kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT Oktoba 13, 2021 na kutakiwa kukamilisha kazi hiyo Novemba 09, 2023 na kutakiwa kukamilisha ujenzi huo uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi.




Discussion about this post