NA MIRIAM SARAKIKYA,ARUSHA
SERIKALI imebaini matishio 459 ya kiusalama mtandao ambapo pia imejipanga kuongeza watumiaji wa interneti kutoka asilimia 43 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha Februari 8,2023 wakati wa kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao (ega) kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi
Akizungumza katika kikao hicho,Ndejembi Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuongeza watumiaji wa interneti kutoka asilimia 43 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2025
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu mwaka 2021 wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, alieleza bayana kuwa serikali itatoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA hususani katika masuala ya utafiti na ubunifu Tehama ili kuwawezesha watanzania kupata huduma bora na kwa wakati kupitia mifumo ya TEHAMA”
“Kupitia TEHAMA Dunia hivi sasa imekuwa ni Kijiji hivyo pamoja na wigo huo pia imejipanga kuongeza kasi ya kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi nchini ikiwemo ngazi za wilaya.
“Tunaitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (ega) kuendelea kufanya tafiti ili kubuni mifumo mipya ya TEHAMA itayoliwezesha taifa kufanikisha kuimarisha sekta ya viwanda na biashara”ameeleza Ndejemi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao(ega)Mhandisi Benedict Ndomba amesema kikao hicho ni cha kipekee kwani ega imetimiza miaka10 na kufanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kubaini matishio ya kiusalama mtandao 459.
Mhandisi Ndomba amefafanua kuwa pamoja na kubaini matishio hayo ya kiusalama lakini pia imefanya ukaguzi na tathmini ya usalama wa mifumo kwa Taasisi za Umma.
Aidha ameongeza kuwa mamlaka hiyo imeendelea kusimamia na kuhimiza uzingatiaji Sera, Kanuni , Sheria na miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi za Umma ili kuhakikisha matumizi ya mfumo wa TEHAMA yanakuwa na tija na ufanisi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felisia Mtahengerwa amebainisha kuwa Mkoa wa Arusha ni moja ya wadau wa Serikali Mtandao kupitia taasisi mbalimbali za umma ambapo wanapata huduma nyingi kwa njia rahisi ,gharama nafuu.




Discussion about this post