NA MWANDISHI WETU,LINDI
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho cha Sh.Milioni 399 kwa wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mohamed Hassan Moyo wakati akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9, 2024 katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
Amesema Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, wananchi zaidi ya 1658 wa wilaya hiyo walipatikana na kugawiwa fedha hizo ambazo zilitoka mwaka 2023 kiasi cha Sh.Milioni 399.4, ambapo wote waliostahili walipatiwa.
”Wilaya yangu imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya mgongano baina ya Binadamu na Wanyamapori na Tembo ndio anayetajwa kuhusika zaidi kwenye migongano hiyo.
”Tembo wanaathiri mali na maisha ya wananchi, lakini pamoja na changamoto hizo kumekuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania(TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.
“Jitihada za TAWA zimefanyika mara nyingi na mimi mwenyewe nimekuwa nikishiriki, jitihada moja ni kwa kutumia helikopta katika kuwaswaga tembo ili warudi hifadhini ,” amesema Moyo

Akizungumzia kuhusu jitihada zinazofanywa na TAWA Katika kukabiliana na migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori Kanda ya Kusini Mashariki, Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni, Linus Chuwa amesema TAWA imeanzisha vituo 10 vya Askari wa kukabiliana na wanyamapori hao ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu na vingine vitano ni vya muda mfupi hasa pale matukio ya wanyamapori hao yanapojitokeza.
Ameongeza kuwa TAWA imenunua gari jipya katika Kituo cha Malola ambalo hutumiwa na Askari wa kituo hicho,kununua ndege nyuki (drones) maalumu kwa ajili ya kuswaga tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kurudisha tembo hifadhini mwaka 2023, zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Chuwa amebainisha kuwa TAWA imepeleka Askari wa Wanyamapori wa vijiji 41 (VGS) katika Chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori ambapo wakati mwingine askari hao hutumiwa na Mamlaka hiyo katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori hao.
Kwa upande wake, Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo mkoani humo ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori na kuwahakikishia wananchi kuwa TAWA iko kazini na inafanya kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile TAWIRI, GIZ na TANAPA.
Aidha Maganja amefafanua kuwa jitihada zingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni viongozi wa makundi na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu




Discussion about this post