TEHRAN,IRAN
RAIS wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Masoud Pezeskhian amesema kuwa maingiliano makubwa ya kiutamaduni baina ya Iran na baadhi ya maeneo ya Tanzania hasa Zanzibar, ni fursa nzuri ya kustawishwa zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.
Rais Pezeskhian amesema hayo Novemba 13,2024 wakati alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyewasili nchini humo kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais huyo wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema, anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 14 wa Iran na kusisitiza kuwa, Tehran iko tayari kustawisha kwa kiwango kikubwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyuga tofauti za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kwa upande wake, Waziri Balozi Kombo,amempongeza Dkt. Pezeshkian kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kumuombea mafanikio katika kazi zake.
Balozi Kombo amesema, uhusiano wa kihistoria baina ya Iran na Tanzania ni wa maelfu ya miaka na kwamba kuna idadi kubwa ya Washirazi wa Iran waliohamia visiwani Zanzibar miaka mingi nyuma na kueneza utamaduni wa Kiirani na hata lugha ya Kifarsi katika maeneo hayo.
Hata hivyo Waziri Balozi Kombo amewakaribisha Wairani kuitembelea Tanzania ili kuzidi kutia nguvu ushirikiano wa mataifa haya mawili katika nyuga tofauti hasa upande wa masuala ya kiuchumi.




Discussion about this post