NA MWANDISHI WETU MOROGORO
WAKAZI wa Kitongoji cha Msondo kilichopo katika Kijiji cha Idondi Halmashauri ya Mlimba mkoani Morogoro wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kuzuia watu wanaovuna mazao yao kwa usimamizi wa polisi kwa kuwa wanateseka na familia zao.
Wananchi hao ambao wamekimbilia katika milima iliyo karibu na kijiji chao kwa hofu ya kukamatwa na Polisi wamesema kwa sasa wanaishi kwa shida kutokana na kushindwa kuvuna mazao yao ambayo waliyapanda wenyewe na kupalilia.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika kijiji hicho, mmoja wa wakulima hao Nyanda Manzabe amesema eneo hilo lilikuwa na mgogoro katika miaka ya nyuma na mtu anayedai kumiliki zaidi ya ekari 1000 kwa jina la Musa.
Amesema tangu mwaka 2021 walichukua hatua za kisheria juu ya mtu huyo anayedaiwa kuwa mwekezaji ambapo mgogoro huo ulifika katika vyombo vya kisheria na mwisho wao waliruhusiwa kulima na kulimiliki eneo hilo.
Amesema baada ya hapo kuanzia mwezi Desemba,2024 walianza kulima na kupanda mazao yao na kuyapalilia vizuri na hakukuwa na kitu chochote lakini ilipofika mwezi Mei,2025 baada ya mazao kuiva na kutakiwa kuvunwa ndipo polisi walipofika na kuanza kuwafukuza.
“Kuna shamba moja lilianza kuiva na tulikwenda kuvuna na familia ya wenye shamba hilo lakini walikuja polisi na kutufukuza,na sisi tulikimbia maana walikuwa na mabomu lakini cha ajabu mazao yetu yakaanza kuvunwa lakini tulipokwenda kufyeka mashamba yaliyoiva sasa hivi wakajana tena polisi wengi zaidi ya wale wa mwanzo na kuvuna mazao yetu.
“Hadi sasa hivi wapo shambani wanavuna mazao yetu,tumuomba Rais samia Suluhu Hassan atusaidie kwenye tatizo hili na sisi tunafamilia na tuko milimani tunaishi kama nyani na hatuna uhuru,sisi tumemalima kihalali lakini iweje sasa hivi tunaanza kuvuna tunavufukuzwa na kisha mazao yetu yanavunwa kwa usimamizi wa polisi”
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hili kwani sisi ni wakulima na tunategemea mazao hayo kulisha familia zetu sasa ikiwa mazao yetu yanavunwa wakati tumelima sisi sasa tutaishije”amesema Manzabe

Mkazi mwingine wa Kijiji hicho ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu za usalama wake,amesema wao wamefanya kazi mshambani na kulima mazao yao lakini wanashangaa kuona polisi wanafika na kuwapokonya chakula chao walicholima na haki walipata kihahali kabisa
“Haki tumepata sisi wananchi lakini bado wamerudi kuwapokonya chakula chao na kilimo ndio kinawakoa ikiwemo kuwalipia ada watoto wao na shule zimeshafungua wao kama wakulina wamewekeza katika kilimo.
“Walitusubiri tulime na kupalilia sasa mazao yetu yameiva wanakuja na polisi kuyavuna hii si sawa tunaomba Rais Samia atusaidie kwani hatuna hata chakula cha kuwalisha watoto lakini kwa nini wavune mazao yetu kwani kama kulikuwa na mgogoro si wangetuzuia kabla ya kulima?tumelima,tumepanda,tumepalilia hadi mazao yamekomaa na sasa yameiva ndio wanakuja polisi kutufukuza halafu wanavuna wao hii sio halali “amesema mama huyo
Juhudi za kuwatafuta viongozi wa eneo hilo zinaendelea baada ya kutafutwa bila mafanikio ili kuzungumzia mgogoro huo.




Discussion about this post