BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji ((EWURA CCC) limesema mtumiaji wa huduma hizo ana haki ya kufidiwa kutokana na kupatiwa huduma mbovu kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopo.
Baraza hilo ambalo limeanzishwa chini ya kifungu namba 30 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya mwaka 2001,Sura ya 414 lina dhamira ya kutetea haki za watumiaji wa huduma za nishati na maji kwa kukuza ufahamu kwa umma.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza hilo leo mkoani Dar es Salaam katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ‘ Uchumu wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’
EWURA CCC imesema kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2021 Baraza hilo imewafikia zaidi ya watumiaji 4200 wa huduma hizo ambapo malalamiko 800 yametatuliwa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtumiaji wa huduma hizo ana haki ya utatuzi mzuri wa madai yake kama hasara imetokana na mtoa huduma.
Aidha imeongeza kuwa mtumiaji wa huduma hizo pia ana haki ya kuelimishwa kuhusu huduma zitolewazo ili kumpa maarifa na ujuzi kumwezesha kuchagua huduma stahiki.
“Haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma hizi ni pamoja na haki ya kufidiwa ,haki ya utatuzi mzuri wa madai,kufidiwa kutokana na kupatiwa bidhaa zenye dosari au huduma mbovu na madai yote ya fidia yazingatie kanuni na taratibu zilizopo”Imefafanua taarifa hiyo.
Mbali na hilo lakini pia mtumiaji wa huduma hizo ana haki na wajibu wa usalama na faragha,kupata taarifa,kuchagua huduma,kusikilizwa, kuwakilishwa na kuwa katika mazingira bora.
“Wajibu wa mtumiaji ni kulipa ankara kwa wakati kwa mujibu wa kanuni,taratibu na viwango vilivyowekwa,kutoa taarifa,kutunza miundombinu na matumizi halali ya miundombinu”imebainisha taarifa hiyo
Discussion about this post